Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres amelaani vikali shambulio lingine dhidi ya raia Niger

Maelfu ya familia wamekimbia makazi yao Magharibi mwa nchi ya Niger kufuatia tishio la mashambulizi ya vikundi visivyofahamika ( Maktaba)
© UNICEF/Islaman Abdou
Maelfu ya familia wamekimbia makazi yao Magharibi mwa nchi ya Niger kufuatia tishio la mashambulizi ya vikundi visivyofahamika ( Maktaba)

Guterres amelaani vikali shambulio lingine dhidi ya raia Niger

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani vikali shambulio lingine tena la watu wasiojulikana wenye silaha dhidi ya raia katika Jamhuri ya Niger lilofanyika Agosti 16 katika eneo la Banibangou, mkoani Tillabéri.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake Katibu Mkuu Antonio Guterres ametuma salamu za pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao.  

Pia amesema ana wasiwasi sana na athari ya kuongezeka kwa mashambulio haya ya mara kwa mara kwa hali ya kibinadamu katika mkoa huo wa Tillabéri, ambako tayari zaidi ya watu 100,000 wamehama makazi yao na wengine 520,000 wanahitaji msaada wa kibinadamu. 

Bwana Guterres ametoa wito kwa mamlaka ya Niger kufanya kila liwezekanalo kuwabaini na kuwafikisha haraka wahusika kwenye mkono wa sheria. 

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kuunga mkono Niger katika juhudi zake za kukabiliana na kuzuia ugaidi na msimamo mkali wa vurugu, kukuza mshikamano wa kijamii na kufikia maendeleo endelevu.