Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkakati wa Mabadiliko ya Kidigitali ya Ulinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa wazinduliwa

Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa raia wa China akiendesha drone ya Video wakati akifanya doria nchini Liberia
UN Photo/Albert Gonzalez Farran
Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa raia wa China akiendesha drone ya Video wakati akifanya doria nchini Liberia

Mkakati wa Mabadiliko ya Kidigitali ya Ulinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa wazinduliwa

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres hii leo katika makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani amezindua ‘Mkakati wa Mabadiliko ya Kidigitali ya Ulinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa’.

Mkakati huu wa mabadiliko ya kidijitali ya ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa unaolenga kuwawezesha walinda amani wa Umoja wa Mataifa kote duniani kuendana sawa na maendeleo ya kidijitali, umezinduliwa na Katibu Mkuu Guterres wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likikutana katika mjadala wa wazi kuhusu ulinzi wa amani  na teknolojia na azimio la kuwalinda walinzi.  

Aidha inaelezwa kuwa mkakati unakusudia kuwezesha ujumbe kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kuimarisha usalama na walinda amani kwa kutumia uwezo wa teknolojia za kidijiti na pia kupunguza hatari, huku ukiweka ulinzi wa amani kuendelea kubadilika katika matumizi yake ya teknolojia. 

Mikakati ya Katibu Mkuu kuhusu Teknolojia Mpya na Takwimu inaweka fursa kwa ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa kutengeneza njia yake kutumia uwezo wa teknolojia katika kusimamia vizuri huduma na mamlaka yake sasa n ahata kwa siku zijazo.

Katika mpango wake wa Ushirikiano wa kidijititali, Katibu Mkuu Guterres anatambua kuwa, "teknolojia za dijitali zinaweza kusaidia juhudi za kulinda amani za Umoja wa Mataifa ulimwenguni, pamoja na kuhakikisha usalama na usalama wa walinda amani." 

Maono ya uwezo zaidi wa ndani wa matumizi ya teknolojia mpya yanaendana na mpango wa Hatua ya Ulinzi wa Amani, A4P; vipaumbele vya A4P Plus, A4P + vya 2021 ambavyo vinasisitiza ulinzi wa amani unaotokana na ubunifu, takwimu na  teknolojia.

Wavuti rasmi wa Ulinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa unaeleza kuwa, “teknolojia za dijitali zinachukua jukumu muhimu na gumu zaidi katika eneo la migogoro. Wanaunda mazingira ya mizozo na wanaathiri tabia na matendo ya watendaji wa mizozo. Teknolojia za kidijitali husababisha hatari mpya lakini pia zinaonesha fursa mpya za kuboresha ufanisi wa shughuli za kulinda amani na usalama na usalama wa walinda amani.”

Kulinda wafanyakazi wa UN 

Na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa pamoja limekubaliana kupitisha azimio la kutaka Nchi Wanachama ambazo ni wenyeji au zimewahi kuwa wenyeji wa operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa kuchukua hatua zote zinazofaa, kwa mujibu wa sheria ya kitaifa na kimataifa, kuwafikisha mahakamani wale wanaowaua au kuwashambulia wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa. 

Tweet URL

Kupitia azimio la 2589 (2021), Mabalozi 15 pia wamemwomba Katibu Mkuu kuanzisha hifadhi au kanzi data kamili ya mtandaoni ya mashambulio dhidi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na walinda amani, inayoweza kupatikana kwa nchi wenyeji, nchi zinazochangia wanajeshi na polisi, na nchi za utaifa wa wafanyakazi ambao ni raia. 

Hafla ya kuwaenzi walinda amani

Kabla ya mjadala huu, Katibu Mkuu Guterres ameshiriki katika hafla ya kutoa heshima kwa huduma na kujitolea kwa walinda amani iliyofanyika katika moja ya bustani za makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia) na Subrahmanyam Jaishankar, Waziri wa Mambo ya nje wa India, katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya New York ya UN kutambua huduma ya walinda amani.
UN Photo/Mark Garten)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia) na Subrahmanyam Jaishankar, Waziri wa Mambo ya nje wa India, katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya New York ya UN kutambua huduma ya walinda amani.

Zaidi ya wanaume na wanawake milioni moja wamehudumu chini ya bendera ya bluu ya Umoja wa Mataifa tangu mwaka 1948, na zaidi ya walinda amani 4,000 wamepoteza maisha yao wakiwa kazini. 

"Kazi yao ya kubwa na kujitolea kwao kabisa hakutasahaulika," Bwana Guterres amesema wakati wa hafla na kuongeza, “leo, walinda amani wetu kwa fahari wanaendeleza heshima ya wale ambao tumewapoteza. Wanaendelea kuleta mabadiliko muhimu katika maisha ya mamilioni ya watu walio katika mazingira magumu zaidi duniani ”.