Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kikosi cha TANZBAT 4 chaenziwa medali CAR kwa uweledi wao

Kikosi cha kulinda amani cha Tanzania nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR wakizungumza na kamanda wa kikosi.
Photo: MINUSCA/Honorine Guehi Niare Yao
Kikosi cha kulinda amani cha Tanzania nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR wakizungumza na kamanda wa kikosi.

Kikosi cha TANZBAT 4 chaenziwa medali CAR kwa uweledi wao

Amani na Usalama

Kikosi cha kulinda amani cha Tanzania nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR kijulikanacho kama TANZBAT4 kimetunukiwa nishani ya utendaji bora katika halma maalum iliyofanyika kwenye eneo la Berberati Magharibi mwa nchi hiyo.

Ni sherehe maalum za kuwatunukia nishani maafisa walinda amani wa  kutoka Tanzania wa kikosi cha 4 au TANZBAT 4 wanaohudumu kupitia mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR uitwao MINUSCA

Kikosi hicho kinachoongozwa na Luteni Kanali Alexander Edward Masangura kiliwasili CAR mwezo Novemba mwaka 2020 Magharibi mwa nchi hiyo na sasa kimehitimisha miezi 9 ya ulinzi wa amani na kutunukiwa nishani ya Umoja wa Mataifa kutokana na weledi wao mkubwa. 

Sherehe hizo zimeambatana na shamrashamra mbalimbali ikiwemo gwaride maalum lililoongozwa na Meja Baraka Songoro. 

Katika hafla hiyo mwakilishi na mkuu wa vikosi vya ulinzi wa amani vya MIUNUSCA Meja Jenerali Paulo Maia Pereira amewapongeza maafisa wa TANZBAT 4 kwa utendaji wao mzuri wenye tija katika shughuli za ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa. 

Itakumbukwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika medani za kimataifa kwenye ulinzi wa amani, ambapo inashiriki katika opereshani mbalimbali duniani ikiwemo hapa CAR, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Darfur Sudan na Lebanon.