Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu wa UN atoa wito kwa pande zote Afghanistan huku  Baraza la Usalama likitegemewa kukutana Jumatatu hii. 

Familia nchini Afghanistan zimekimbia nyumba zao kutokana na mgogoro na sasa wanaishi katika kambi mjini Kandahar
© UNICEF Afghanistan
Familia nchini Afghanistan zimekimbia nyumba zao kutokana na mgogoro na sasa wanaishi katika kambi mjini Kandahar

Katibu Mkuu wa UN atoa wito kwa pande zote Afghanistan huku  Baraza la Usalama likitegemewa kukutana Jumatatu hii. 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anafuatilia hali ilivyo huko Afghanistan akiwa na wasiwasi mkubwa na amewasihi Taliban na wahusika wote wajizuie kwa kiwango cha juu ili kuepusha madhara kwa raia na pia kuhakikisha utoaji wa misaada ya kibinadamu. 

“Mzozo huo unalazimisha maelfu ya watu kuondoka katika nyumba zao. Kuna ripoti zinazoendelea za ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika jamii zilizoathiriwa na mapigano.” Imesema taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa na msemaji wake, Stephane Dujarrick mjini New York Marekani Jumapili.  

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, Jumapili hii Wataliban ambao tayari wanadhibiti sehemu kubwa ya Afghanistan, wameingia katika mji mkuu, Kabul, wakati Rais Ashraf Ghani na maafisa wengine wakitoroka nchini. 

Katibu Mkuu Guterres ametoa wito kwa Taliban na pande zote kutii kanuni za sheria za kimataifa za kibinadamu, na kulinda na kuheshimu haki na uhuru wa raia wote. 

"Katibu Mkuu ana wasiwasi hasa juu ya mustakabali wa wanawake na wasichana, na haki zao ambazo zilipatikana kwa taabu lazima zilindwe." imesema taarifa hiyo. 

Umoja wa Mataifa pia umetangaza utayari wake wa kutoa msaada wa kibinadamu kwa Waafghan wote wali katika uhitaji 

Aidha Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza akisema, "Katibu Mkuu anatoa wito kwa pande zote kuhakikisha kuwa mashirika ya kibinadamu yanapata fursa pasina kipingamizi kwa ajili ya upatikanaji wa msaada muhimu kwa wakati."  

Jumatatu hii ya Agosti 16, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atazungumza na wajumbe wa Baraza la Usalama, ambalo litakutana katika mkutano kuhusiana na hali hiyo nchini Afghanistan.