Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali si shwari Afghanistan, sitisho la mapigano ndio muarobaini 

IOM inasaidia familia zilizofurushwa nchini Afghanistan, ikitoa makazi ya dharura na ulinzi.
IOM/Mohammed Muse
IOM inasaidia familia zilizofurushwa nchini Afghanistan, ikitoa makazi ya dharura na ulinzi.

Hali si shwari Afghanistan, sitisho la mapigano ndio muarobaini 

Wahamiaji na Wakimbizi
  • Mapigano yamesambaa katika majimbo 33 kati ya 34 
  • Wanaoathirika zaidi ni wanawake na watoto 
  • Nchi jirani na Afghanistan fungueni mipaka yenu 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia UNHCR, linatiwa hofu kubwa na janga la kibinadamu linaloendelea kuibuka huko Afghanistan kila uchao. 

Kadri mapigano yanavyoendelea kusambaa, Umoja wa Mataifa nao unazidi kutoa wito wa sitisho la kudumu la mapigano na makubaliano ya kusaka suluhu ya kudumu kwa maslahi ya wananchi wote wa Afghanistan. 

Kauli hizo zimetolewa leo huko mjini Geneva, Uswisi na msemaji wa UNHCR Babar Baloch wakati akizungumza na waandishi wa habari, wakati huu ambapo tayari naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema anafuatilia kwa karibu kile kinachoendelea katika taifa hilo la Asia. 

Tweet URL

Bwana Baloch amesema, “ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA umeonya kuwa bila kumalizika kwa ghasia Afghanistan inaelekea kwenye hali ya kushuhudia idadi kubwa ya vifo vya raia kuwahi kusajiliwa kwa mwaka mmoja tangu Umoja wa Mataifa uanze kuweka kumbukumbu hizo.” 

Amesema hofu kubwa ni madhara ya mapigano hayo kwa wanawake na watoto wa kike akisema kwamba tarkibani asilimia 80 ya robo ya wananchi wote wa Afghanistan waliolazimika kukimbia makazi yao tangu mwezi Mei mwaka ni wanawake na watoto. 

Halikadhalika Takribani watu laki nne wamelazimika kukimbia makwao tangu mwanzoni mwa mwaka huu na kuongeza katika idadi ywa waafghanistani milioni 2.9 ambao tayari walikuwa wakimbizi wa ndani nchini humo mwishoni mwa mwaka jana wa 2020. Mapigano yameripotiwa katika majimbo 33 kati ya majimbo yote 34 ya Afghanistan  

Zaidi ya yote tangu mwanzoni mwa mwakahuu, takribani raia 120,000 wa taifa hilo wamekimbia maeneo ya vijiji na kuelekea jimbo la Kabul. 

“UNHCR inasihi jamii ya kimataifa ichukue hatua za haraka kusaidia kushughulikia janga hili la sasa la ukimbizi Afghanistan. Timu zetu ikiwa ni miongoni mwa juhudi pana za Umoja wa Mataifa, zimetathmini mahitaij ya wakimbizi 400,000 mwaka huu na zinasambaza mahitaji ya dharura kama vile maji, chakula, malazi, huduma za kujisafi na vikasha vya huduma nyeti kwa wanawake na wasichana,” amesema Bwana Baloch. 

Amekumbusha kuwa shirika hilo linatoa wito kwa nchi jirani na Afghanistan zifungue mipaka yao wakati huu ambapo mapigano yanazidi kushamiri.