Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake na wasichana waendelea kubakwa huko Tanganyika, DRC

Msichana akiwa amembeba mdogo wake katika mji wa Kalemie, jimbo la Tanganyika,DRC
Picha na UNICEF/Vockel
Msichana akiwa amembeba mdogo wake katika mji wa Kalemie, jimbo la Tanganyika,DRC

Wanawake na wasichana waendelea kubakwa huko Tanganyika, DRC

Wahamiaji na Wakimbizi

•    Matukio 17 ya ubakaji kila siku jimboni Tanganyika, miongoni mwa wanaobakwa ni watoto.
•    Vikundi vyenye silaha vinagombea machimbo ya madini
•    UNHCR yataka usalama ili manusura wapatiwe huduma za afya

Jimboni Tanganyika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC matukio ya kupangwa ya ukatili wa kingono dhidi ya wanawake, wasichana na watoto wa kike yameripotiwa kuongezeka, jambo linalotia hofu kubwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.

Msemaji wa UNHCR mjini Geneva, Uswisi, Babar Baloch amewaeleza waandishi wa habari kuwa vitendo hivyo vinavyofanywa na makundi yaliyojihami jimboni humo wakati huu ambapo maelfu ya watu wamefurushwa makwao mwaka huu kutokana na mapigano baina ya makundi yanayogombania machimbo ya madini.

Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya watu 23,000 wamekimbia kutoka mji wa Kongolo ulioko kaskazini mwa jimbo la Tanganyika tangu mwezi Mei mwaka huu na kati yao wameshakimbia makwao mara tatu.

Katika wiki mbili tu pekee zilizopita, wadau wa kibinadamu katika kanda za kiafya za Kongolo na Mbulula wamerekodi matukio 243 ya ubakaji, ambapo visa 48 ni dhidi ya watoto katika vijiji 12, ikiwa in wastani wa matukio 17 kwa siku.

Hata hivyo Bwana Baloch anasema, “takwimu za ukatili wa kijinsia zinaweza kuwa kubwa zaidi kwa kuwa bado katika jamii nyingi suala hili ni siri na halipaswi kusemwa. Halikadhalika, kuna tatizo la saikolojia na kiwewe kutokana na kubakwa, na kwamba manusura wa ubakaji wanaweza kukabiliwa na unyanyapaa au kutengwa na familia zao.”

Kutokana na mapigano baina ya makundi yenye silaha yanayogombania machimbo ya madini, huku vikosi vya serikali vikijibu mashambulizi, raia wanajikuta katikati ya mvutano wa makundi hayo.

“Wafanyakazi wetu wamesikiliza shuhuda za kutisha za ukatili. Wakimbizi wa ndani wameshutumu vikundi vilivyojihami kwa kubaka wanawake ambao wanajaribu kukimbia makazi yao. Baadhi ya wanawake na wasichana wametekwa na kutumika kama watumwa wa kingono na vikundi hivyo vilivyojihami.” Babar Baloch, UNHCR

Kwa wale wanaoataka kukombolewa, makundi hayo yanadai kikombozi kutoka kwa familia.

UNHCR na wadau wake wanaendelea hata hivyo kufanya kazi na serikali za maeneo hayo na wahudumu wa kibinadamu ili kuhakikisha kuna usaidizi wa kisaikolojia na kitabibu kwa manusura wa ubakaji, lakini tatizo bado ni usalama kwa kuwa kuna umbali mrefu kufikia vituo vya afya.

Msemaji huyo amerejelea wito wa UNHCR kwa mamlaka kuimarisha usalama kwenye eneo hilo linalojulikana utatu wa kifo, eneo ambalo linapalaka na maeneo ya jimbo la Tanganyika na jimbo la Kivu Kusini, usalama ambao utatoa hakikisho kwa raia hususan wanawake na wasichana.
Halikadhalika usalama ambao utawezesha wahudumu wa kibinadamu kufikia wahitaji na pia uchunguzi wa watekelezaji wa vitendo hivyo ili wafikishwe mbele ya sheria.

Hati mwezi uliopita wa Julai, takribani watu 310,000 wamefurushwa makwao jimboni Tanganyika kutokana na ghasia.

Mahitaij ya kibinadamu nayo yameongezeka huku ombi la UNHCR la dola milioni 205 za kusaidia operesheni zake nchini humo likiwa limefadhiliwa kwa asilimia 36 pekee.