Guterres afuatilia hali ya usalama Afghanistan

12 Agosti 2021

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anafuatilia kwa karibu na kwa wasi wasi mkubwa kile kinachoendelea nchini Afghanistan, ikiwemo ripoti za mapigano makali kwenye jimbo la Herat na Kandahar.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani hii leo, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema Katibu Mkuu ana wasiwasi mkubwa zaidi na kitendo cha mapigano kuhamia maeneo ya mjini ambako raia wengi zaidi wako hatarini. "Tunatumai kuwa majadiliano ya wiki hii huko Doha, Qatar kati ya wawakilishi wa serikali ya Afghanistan na wale wa kikundi cha Taliban sambamba na wajumbe wa kikanda na kimataifa yaaweza kurejesha njia ya kuanza upya mazungumzo na pia kuweza kuweka fursa ya usaidizi kwa wananchi wa Afghanistan.”

Kuhusu hali ya kibinadamu amesema “naweza kuwaeleza kuwa watu wengi wanawasili kwenye mji mkuu Kabul na miji mingine mikubwa wakisaka usalama kutokana na ghasia na vitisho huko wanakoishi.”

Pamoja na ghasia mashirika ya misaada yanaendelea na huduma zao nchini humo ambapo Bwana Dujarric amesema, “watu milioni 18.4 wakihitaji msaada wa kibinadamu, na mgogoro ukisababisha watu 390,000 mwaka huu pekee kufurushwa makwao bado wahudumu wa kibinadamu wako Afghanistan.”

Tathmini ya mashirika mbalimbali inaendelea maeneo mbalimbali ikimulika ukimbizi kutokana na ghasia, mizozo, chakula, masuala ya jinsia na ulinzi na wakati huo huo kubaini mahitaji ya kibinadamu na mengineyo.

Bwana Dujarric amesisitiza kuwa mashirika ya kutoa misaada na Umoja wa Mataifa wanaendelea kusalia nchini humo kusaidia raia wananchi wa Afghanistan licha ya hali ya usalama kusalia ni ngumu.
 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter