Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Simulizi: Kutoka maisha ya ghasia hadi utamaduni wa amani 

Vijana nchini Cameroon ni kiungo muhimu katika kuchagiza amani Afrika Mgharibi
© UNICEF/Salomon Marie Joseph Beguel
Vijana nchini Cameroon ni kiungo muhimu katika kuchagiza amani Afrika Mgharibi

Simulizi: Kutoka maisha ya ghasia hadi utamaduni wa amani 

Amani na Usalama

Nchini Cameroon, kijana mwanaharakati ambaye amegeuza maisha yake kutoka yale ya vurugu na ghasia hadi kuwe kijana mtetezi wa masuala ya raia na amani kwenye jamii yake amezungumza na Umoja wa Mataifa na kuelezea jinsi ambavyo anasaidia vijana wengine kukataa mizozo na badala yake wachukue dhima kubwa ya kujenga amani nchini mwao. 

Christian Achaleke amezungumza na Umoja wa Mataifa mapema kabla ya maadhimisho ya leo ya siku ya kimataifa ya vijana ambayo hufanyika tarehe 12 ya mwezi Agosti kila mwaka. 

 “Uamuzi wangu wa kuwa mwanaharakati wa amani umechochwa na uzoefu wangu binafsi. Nimekulia katika jamii iliyozongwa na ghasia: ilikuwa ndio sehemu ya maisha ya kila siku. Kuna wakati, nilibaini kuwa fujo na ghasia havitatupeleka popote. Nilipoteza rafiki zangu wa karibu na wengine waliswekwa gerezani.” 

Nilianza shughuli za kujitolea mwaka 2007, na hii ilinipatia mtazamo mpya kuhusu amani na kusaidia kuimarisha jamii. Kimekuwa ni kitu cha hamasa kubwa na uzoefu wa kubadilisha maisha yangu. 

Christian Achaleke akihutubia jamii katika maeneo yalioathiriwa na mzozo kusini magharibi mwa Cameroon.
LOYOC Cameroon
Christian Achaleke akihutubia jamii katika maeneo yalioathiriwa na mzozo kusini magharibi mwa Cameroon.

 Kama kijana ninayehusika na ujenzi wa amani na kukabiliana na misimamo mikali inayosababisha vita, najikuta mara kwa mara nazungumza na watu wa rika langu. Pindi nitembeleapo magereza kuzungumza na vijana, naweza kuwaonesha kuwa kuna fursa bora zaidi za kushughulikia changamoto zinazowakabili badala ya kutumia fujo na hivyo tunasaka suluhu za vichocheo vya mizozo. 

Uwezo wa vijana hupuuzwa 

Hata hivyo, naweza kusema kuwa dhima yetu huwa inapuuzwa. Wakati mwingine nahisi jamii, viongozi na taasisi zinafumbia macho kile ambacho tunafanya, hata kama sisi ndio ambao tunaathirika mara nyingi wakati wa mizozo.  

Nchini Cameroon, tumejaribu kupatia vijana fura ya kushirikiana na jamii katika ujenzi wa amani na harakati za michakato ya amani, kwa kuwapatia miongozo, misaada na mafunzo ya kuinua uwezo wao.  

Tunaiambia serikali, Umoja wa Mataifa na mashirika mengine kuwa ni mkakati mzuri wa kujumuisha vijana, kuwapatia stadi na kushiriki katika usuluhishi na kuwapatia nafasi salama ambamo wanaweza kushiriki kwenye mchakato huo.  

Vijana wengi nchini Cameroon wamekimbia makazi yao kutokana na vita na sasa wanaishi katika kambi za wakimbizi wa ndani.
© UNHCR/Xavier Bourgois
Vijana wengi nchini Cameroon wamekimbia makazi yao kutokana na vita na sasa wanaishi katika kambi za wakimbizi wa ndani.

Utamaduni, utofauti na urithi ni mambo muhimu sana kwangu kama rai awa Cameroon. Vinapaswa kuwa vitu vya kutuunganisha, lakini kwa sababu hatukutumia fursa nzuri kuvuna faida zake, sasa tunakumbana na mizozo mikali. 

Ndio maana kusimamia utamaduni, urithi na utofauti na jamii ya wengine walioko ughaibuni ni jambo muhimu sana kwa ajili ya amani, n ani kitu ambacho tumekuwa tunajaribu kufanya kwa muda mrefu. 

Maadili ya kuzuia mzozo 

 Maadili na tabia vinaweza kusaidia kuongoza utamaduni wa amani, kwa mujibu wa Christian Achaleke.
UN News/Daniel Dickinson
 Maadili na tabia vinaweza kusaidia kuongoza utamaduni wa amani, kwa mujibu wa Christian Achaleke.

Kwangu mimi, utamaduni wa amani ni seti nzima ya maadili, mfumo wa maisha, tabia ambavyo vinaendelezwa kama njia ya kuzuia ghasia au vita na pia kujumuisha watu kuelekea katika maisha ya amani na yenye maadili. 

Kujenga utamaduni wa amani Afrika, vijana na wanawake wanapswa kushirikishwa, na kuwa mstari wa mbele wa mchakato huo. Ni muhimu pia kupatia fursa watu na jamii ili waweze kuelezea uzoefu wao na kutoa mawazo. 

Ni mambo machache sana yanazungumzwa kuhusu vijana wanaobadilisha taswira ya bara la Afrika, lakini hii haimaanishi kuwa hatufanyi kazi nzuri. Natoa wito kwa viongozi wa serikali, watunga sera, jamii na kila mtu mwenye nia njema kusimama kidete na kusaidia vijana wa kike na wa kiume na kuhakikisha kuwa wanaweza kuongoza marekebisho ndani na zao na kujenga bara la Afrika.”