Malembo Farm yajizatiti kuwainua vijana kwenye kilimo nchini Tanzania

Wanafunzi nchini Tanzania wanaohudhuria darasa la kilimo
Malembo Farm Academy
Wanafunzi nchini Tanzania wanaohudhuria darasa la kilimo

Malembo Farm yajizatiti kuwainua vijana kwenye kilimo nchini Tanzania

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ikiwa leo ni siku ya vijana duniani, Umoja wa Mataifa unapigia chepuo ushiriki wa vijana katika kuimarisha mifumo ya chakula duniani kwa kuzingatia kuwa miaka 30 ijayo watu bilioni 2 zaidi wataongezeka duniani na kuongeza mahitaji ikiwemo ya chakula.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake wa siku hii ya vijana, anawataka vijana wachukue hatua na miongoni mwao ni mmiliki wa taasisi moja nchini Tanzania inayoshirikisha vijana kwenye kilimo.

Mifumo sahihi ya chakula ni suluhisho la upatikanaji wa chakula na ushiriki wa vijana ndio nguzo muhimu na ndio maana taasisi ya Malembo Farm nchini Tanzania imeitikia wito wa Umoja wa Mataifa wa vijana kuchukua hatua kama alivyonieleza Mkurugenzi wake, Lucas Malembo. “Malembo Farm academy imeanza mwaka 2020, na tumeanza na wanafunzi wa shule tatu za sekondari jijini Dar es Salaam walio kidato cha 5 na sasa wamemaliza ni kidato cha 6. Tulianza na vijana 15 na tumekuwa nao katika darasa la kilimo kila jumamosi, siku ambayo wanakuwa mapumziko hawaendi shuleni na wanakuja katika taasisi yetu kujifunza mambo ya kilimo kwa ujumla. Kwakweli tumeona mabadiliko kwa vijana hawa kwani wameanza kilimo majumbani mwao na wameelewa kilimo ni eneo la biashara.” 

Janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19, limeathiri wakulima kwa kupandisha bei za pembejeo na maeneo mengine nyeti na hivyo ubunifu wa vijana katika nyanja hiyo umeonekana kuwa muarobaini. Malembo Farm imebisha hodi kwa wabunifu walioko Vyuo Vikuu. 

“Tumeanzisha kampeni ya Nyoto yangu university ( chuo kikuu), lengo ni kutembelea vyuo vikuu na kueleza fursa zilizopo kwenye kilimo, tumefanya kampeni hii katika chuo cha sayansi na kilimo kilichopo mkoani Mbeya na pia tumeenda katika vyuo vingine vidogo na vyuo vya kati , lengo letu ni kuwashawishi vijawa wajiajiri kupitia kilimo.” 

Kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya vijana kimataifa ni “kubadili mifumo ya chakula: ubunifu wa vijana kwa afya ya binadamu.