Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dawa aina 3 kujaribiwa kwa wagonjwa mahututi wa COVID-19

Mwanasayansi wa maabara akifanya utafiti katika kituo cha ushirikiano cha utafiti cha WHO nchini Thailand
© WHO/Ploy Phutpheng
Mwanasayansi wa maabara akifanya utafiti katika kituo cha ushirikiano cha utafiti cha WHO nchini Thailand

Dawa aina 3 kujaribiwa kwa wagonjwa mahututi wa COVID-19

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO limetangaza litaanza majaribio ya dawa aina tatu kwa ajili ya kuwatibu wagonjwa walio mahututi kutokana na ugonjwa wa Corona au COVID-19. 

Katika mkutano wake na vyombo vya Habari mjini Geneva, Uswisi Mkurugenzi Mkuu wa WHO DKT. Tedrosa Adhanom Ghebreyesus amesema kupitia mpango wa mshikamano wa majaribio ya dawa za kutibu Corona uliopewa jina na Solidarity Plus watafanya majaribio dawa aina tatu katika nchi 52. 
 
Dawa hizo zitakazo fanyiwa majaribio ni ARTESUNATE, AMATINIB na INFLIXIMAB ambazo zilichaguliwa na jopo huru la wataalamu waliokuwa wanaangalia namna ya kusaidia kupunguza vifo mahospitali vya wagonjwa wa COVID-19
 
"Kupata tiba bora na inayoweza kupatikana kwa wagonjwa wa COVID-19 bado ni hitaji muhimu, na WHO inajivunia kuongoza juhudi hii ya ulimwengu," amesema Dk Tedros na kuongeza kuwa "ningependa kuzishukuru serikali zinazoshiriki, kampuni za dawa, hospitali, waganga na wagonjwa, ambao wamekuja pamoja kufanya hili kwa mshikamano wa kweli wa ulimwengu." 
 
Dawa hizo ambazo zimetolewa bure kwa ajili ya majaribio na wazalishaji wake si mpya kwani zimekuwa zikitumika katika kutibu magonjwa mengine. Artesunate inatumika kutibu malaria kali, Imatinib inatumika kutibu baadhi ya saratani, na Infliximab inatumika kwenye magonjwa kadhaa ya mfumo wa kinga pamoja na ugonjwa wa damu.  

Kampuni zilizotoa dawa hizo kwa ajili ya majaribio ni Ipca, Novartis na Johnson&Johnson. 
 

  Solidarity PLUS 

Kupitia jukwaa la Solidarity PLUS watafiti kote ulimwenguni wana nafasi ya kutumia utaalamu wao na rasilimali kuchangia utafiti wa ugonjwa COVID-19 unaokabili dunia. 
Jukwaa la majaribio Solidarity PLUS ni jukwaa ambalo linawakilisha ushirikiano mkubwa zaidi ulimwenguni kati ya nchi wanachama wa WHO na linahusisha maelfu ya watafiti katika hospitali zaidi ya 600 katika nchi 52. 
 
Uwepo wa jukwaa hili unaruhusu majaribio kutathmini matibabu anuwai kwa wakati mmoja kwa kutumia itifaki moja, kujumuisha maelfu ya wagonjwa, kutoa makadirio thabiti juu ya athari ambayo dawa inaweza kuwa nayo juu ya vifo na pia hata athari za wastani. 
 
Halikadhalika, kupitia Solidarity PLUS, watafiti kote ulimwenguni wana nafasi ya kutumia utaalamu wao na rasilimali kuchangia utafiti wa COVID-19 unaogharimu maisha ya maelfu ya watu ulimwenguni. 
 
Hapo awali, dawa aina 4 zilifanyiwa majaribio na jukwaa hilo na matokeo ya utafiti huo yalionesha kuwa Remdesivir, Hydroxychloroquine, Lopinavir na Interferen zilikuwa na athari kidogo au hakukuwa na madhara kabisa kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini wakiugua COVID-19 
 
Jukwaa hili lenye nchi 52 limekuwa na ongezeko la nchi 16 zaidi ya awamu kwenye majaribio ya kwanza.