Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Masoko maalumu ya kimkakati nchini Tanzania yana mchango chanya katika mifumo ya chakula - FAO 

Nafaka sokoni
UNMISS/James Sokiri
Nafaka sokoni

Masoko maalumu ya kimkakati nchini Tanzania yana mchango chanya katika mifumo ya chakula - FAO 

Ukuaji wa Kiuchumi

Utambuzi wa masoko ya kimkakati nchini Tanzania unaofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika jamii, umeleta mafanikio katika mifumo ya chakula kwani masoko hayo yanarahisisha kuweka mazingira bora ya kukutanisha wauzaji na wanunuzi.

Masoko maalumu yaliyokaa kimkakati, ni maeneo maalumu ambapo wauzaji ambao pia kwa kiasi kikubwa ni wazalishaji wa mazao katika eneo fulani la nchi wanakutana na wanunuzi. Nchini Tanzania, moja ya masoko hayo ni Soko la Kibaigwa lililoko mkoani Dodoma katikati mwa nchi.  Jeremia Mwembe Maina ni mmoja wa wakulima wanufaika wa soko hili anasema, 

“Faida kubwa ninayoipata, umuhimu wa peke yake, kwanza, navuna alizeti mapema, nahakikisha watoto wangu wanaosoma ninakidhi mahitaji yao. Baadaye ninavuna mahindi kama chakula na ninavuna mbaazi kwa ajili ya kuandaa kilimo kijacho. Faida ninayoipata katika kuuza kwenye sokpo la Kibaigwa, ni usalama na uhakika. Ninauza, ninapata hela yangu taslimu, ninaenda kufanya jambo langu ambalo linanihusu.” 

Masoko kiujumla, ndio msingi wa mifumo ya chakula na ni muhimu kuhakikisha kuwa chakula bora na cha aina mbalimbali kipo na kinapatikana. Gledis Mihamb yeye ni miongoni mwa wateja wanaonufaika na uwepo wa soko la Kibaigwa anaeleza akisema,  “Soko la Kibaigwa lina ubora mwingi sana kutegemeana na jinsi akina mama tunavyojishughulisha, tunavyopata vyakula kutoka karibu.” 

Hatua zinazolenga wanawake wanaofanya shughuli katika masoko haya ni muhimu. Nchini Tanzania, wanawake wanakumbana na ugumu kiasi fulani katika kunufaika na kazi yao kwenye masoko haya maalumu. Hili linadhihirika katika tofauti ya kipato kati ya wanaume na wanawake. Esther Masinga mchuuzi mdogo sokoni Kibaigwa anasema,  “Labda kama nitapewa mkopo hapo bishara yangu itaongezeka iwe kubwa ili niweze kupata faida kubwa. Hapa napata hiyo hela kiswango kidogo kutokana na kuwa mtaji ninao mdogo. Mtaji ukiwa mkubwa na hela inakuwa kubwa ya faida.”  

Utambuzi wa masoko maalumu nchini Tanzania tayari umesaidia kuonesha fursa za uwekezaji lakini unaweza kufanya zaidi kuelekea katika ustawi bora na mifumo endelevu ya chakula.