Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake wa jamii za asili Venezuela wajizatiti kulinda msitu wao

Jamii ya watu wa asili wanalinda msitu kama huu.
CIFOR/Terry Sunderland
Jamii ya watu wa asili wanalinda msitu kama huu.

Wanawake wa jamii za asili Venezuela wajizatiti kulinda msitu wao

Tabianchi na mazingira

Wanawake wa jamii ya asili katikati ya msitu wa hifadhi wa Imacata nchini Venezuela wamechukua jukumu la kulinda ardhi yao iliyoathiriwa kwa miaka mingi kutokana na shughuli za madini na ukataji miti. Shirika la Umoja wa Mataifa la kilimo na chakula FAO limeunga mkono juhudi za wanajamiii hao kwa kutoa miche ya kurejesha uoto wa asili.

Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO ikionesha taswira ya ukijani uliokolea wa msitu wa hifadhi wa Imataca ulioko Kusini mashariki mwa Venezuela unaokaliwa na jamii ya Karina ambayo kwa muda mrefu umeathiriwa na shughuli za ukataji miti pamoja na madini hadi  pale, wanawake wa jamii za asili walipoamua kumchagua kiongozi mpya wa kusimamia ardhi hiyo ambaye amepewa cheo cha Kapteni Jenerali. 

Cheo amepatiwa Cecilia Rivas mwanamke ambaye si tu anataka kurejesha bayoanuai ya msitu wao lakini pia anataka kila mtu achape kazi na kuinua kipato cha wananchi, tegemeo lake kubwa likiwa ni kwa wanawake. 

"Wanawake ndio wenye nguvu hivi sasa hivi katika jamii ya Botanamo, kwa sababu nadhani wana ushiriki mkubwa na wana motisha. Ukiwaita tu , waitika mara moja. ” 

Miongoni mwa shughuli alizofanya tangu ashike wadhifa wa kusimamia msitu huu mwaka 2016 ni pamoja na kuomba umiliki wa ardhi kutoka serikalini  ambapo walipatiwa hekari elfu  7 na kisha kupata msaada wa miche ya kupanda kwenye zaidi ya hekari 1,400 kutoka FAO. 

"Tulizungumza na dada zetu na kaka zetu wa jamii za asili, na tukakubalia, iwe sisi si wamiliki wa msitu au ni wamiliki, lakini muhimu zaidi ni kuwa sisi ndio tunaoishi katika hifadhi hii ya msitu wa Imataca, hivyo tunaweza kuunda kampuni yetu ya kuuza mazao kama asali, samaki na kushirikiana na serikali kulinda mazingira yasiharibike” 

Ari hiyo ikawatuia FAO na mkuu wa kitengo cha watu wa jamii ya asili Yon Fernandez-de Larrinoa ambaye anasema wana matumani makubwa na mchango unaotolewa na jamii za watu wa asili. 

 "Tunachoona katika utafiti ambao tunafanya, katika ushahidi tunaokusanya kutoka mashinani na ulimwenguni kote, ni kuwa takwimu zinaonesha watu wa jamii za asili ndio wanabadilisha taswira ya mchezo, wao ndio wanaleta uendelevu, na wanastahimili, na hii sio maneno matupu tu, wamekuwa wakitumia mifumo hii ya chakula ya asilia kwa miaka mingi, na wamekuwa wakizalisha chakula bila kuharibu maliasili kwa miaka yote. ” 

Kwa sasa chini ya uongozi wa kapteni generali Cecilia wananchi wa Karina wanawake kwa wanaume wamefungua kampuni ya Tukupu inayohusika na kurejesha uoto wa asili, kushughulikia na athari za uchimbaji madini pamoja na upandaji miti katika vitalu vilivyosambazwa katika jamii zote bila kusahau kufufua ufugaji wa samaki aina ya Tukupu ambaye amepewa jina la kampuni yao.