Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia inapaswa kuheshimu jamii za asili: Guterres

Sarah Curruchich akiwa ameshikilia kikapu chenye mahindi
Xun Ciin
Sarah Curruchich akiwa ameshikilia kikapu chenye mahindi

Dunia inapaswa kuheshimu jamii za asili: Guterres

Utamaduni na Elimu

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya jamii za asili, dunia imehimizwa kuonesha mshikamano wa kweli na kufanya kazi kwa pamoja katika kuhakikisha kunakuwa na usawa kwa watu wa asili, kutambua dhuluma wanazovumilia, na kusherehekea maarifa na hekima zao.

 Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antoni Guterres kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo mjini Newyork, Marekani.

“Watu wa asili ulimwenguni kote wameendelea kukabiliana na kutengwa, kubaguliwa kwa sababu za kikoloni na mifumo dume bila ya kuheshimu haki zao, utu, na uhuru wao wa kiasili. Wamekuwa wakiporwa ardhi, mipaka, haki za kisiasa na kiuchumi wao na watoto wao, na pia tamaduni na lugha zao zimekuwa zikidharauliwa na kuzimwa.”

Guterres amesema katika miezi ya hivi karibuni dunia imeshuhudia matendo mabaya wanayofanyiwa watu wa asili na wakoloni. Japo kuna mataifa yameanza kushughulikia kasoro hizo na kuomba msamaha, kurekebisha sheria na katiba zao, lakini bado kuna mengi yanahitajika kufanyika. “Tunahitaji kurejesha jamii mpya- jamii ambayo itaheshimu haki, utu, na uhuru wa wale ambao wamenyimwa haki hiyo kwa muda mrefu. Lazima kuwe na majadiliano ya kweli yanayoruhusu kusikilizana. Tayari kuna juhudi zimefanyika katika kuwezesha hili ikiwemo Azimio la Umoja wa Mataifa la haki za watu wa asili, na hati ya matokeo ya mkutano wa ulimwengu wa watu wa asili.”

 Idadi ya watu wa asili duniani 

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa duniani kote kuna jumla ya watu wa asili milioni 476. Watu hawa wote wanastahili kujitawala na kushiriki katika kufanya maamuzi yote, na kutekeleza maono yao ya maendeleo.

Wakati dunia ikiendelea kuongeza uelewa na kuwatambua watu wa asili, Guterres amehimiza changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wa asili kama vile mabadiliko ya tabianchi, kuathirika kwa baianoai katika maeneo yao, pamoja na kuibuka kwa magonjwa ya maambukizi lazima utatuzi wa changamoto hizo uzingatie maarifa ya asili ya watu hao, na kuwashirikisha wenyeji kwenye maamuzi.