Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Joto lazidi kuongezeka duniani, binadamu anyooshewa kidole

Moto wa nyika katika hifadhi ya taifa ya Oregon, nchini Marekani
Unsplash/Marcus Kauffman
Moto wa nyika katika hifadhi ya taifa ya Oregon, nchini Marekani

Joto lazidi kuongezeka duniani, binadamu anyooshewa kidole

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema zinahitajika nguvu za pamoja kutoka kwa viongozi wote wa serikali duniani na kwa haraka sana ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoikabili dunia baada ya ripoti mpya ya wanasayansi kuhusu mabadiliko ya tabianchi IPCC iliyotolewa leo kubainisha kuwa shughuli za binadamu zinapeleka dunia katika madhara ya tabianchi yasiyorekebishika. 

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo mjini New York, Marekani kuhusu uchambuzi wa ripoti hiyo, Guterres amesema, ripoti imeonesha shughuli za kibinadamu zinazidi kuiathiri sayari dunia na joto limezidi kuongezeka ilihali kuna makubaliano yaliyofanyika Paris ya nchi zote kupunguza gesi ya ukaa.

“Ripoti ya leo ya IPCC imeonesha alama ya hatari, shughuli za kibinadamu zinaendelea kuathiri dunia na haziwezi kukanushwa kwani kuna ongezeko la uzalishaji wa gesi ya ukaa, ukataji wa miti na shughuli zote hizi zinawaweka mabilioni ya watu katika hatari. Joto limeathiri kila kona ya dunia na mabadiliko mengi hayatabiriki.”

Akizungumzia mkataba wa kimataifa wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi uliopitishwa mwaka 2015, Guterres amesema, “kwa sasa tupo kwenye nyuzi joto 1.2 katika kipimo cha Selsiyasi na joto lingali likiongezeka kwa haraka huku viwango vya gesi chafu navyo vikiongezeka, hali mbaya ya hewa na majanga mengine pia yakiongezeka. Kizingiti tulichokubaliana kimataifa cha nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi kiko karibu sana kufikiwa na hii ni hatari na lazima tuchukue hatua sasa.”

Shule ilioko mkoa wa Bujumbura vijijini ambapo mafuriko yamekatiza shughuli za masomo.
IOM 2021/Triffin Ntore
Shule ilioko mkoa wa Bujumbura vijijini ambapo mafuriko yamekatiza shughuli za masomo.

Kila mtu yupo hatarini 

Ripoti hii imeandaliwa na wanasayansi 234 kutoka nchi 66, ikimulika jinsi binadamu amesababisha ongezeko la joto duniani katika kiwango kisicho cha kawaida katika miaka 2,000 iliyopita.
Mwaka 2019, viwango vya hewa ya CO2 vilikuwa juu kuliko wakati wowote katika miaka angalau milioni 2 iliyopita na viwango vya hewa aina ya methane na Naitrate Oksaidi navyo vilikuwa vya juu kuliko miaka 800,000 iliyopita.
Viwango vya joto duniani vimeongezeka haraka tangu mwaka 1970 kuliko miaka 50 kwa angalau miaka 2,000 iliyopita. Mathalani kiwango cha joto katika muongo wa hivi karibuni zaidi 2011hadi 2020 kilivuka kile cha karne za hivi karibuni zaidi, takribani miaka 6,500 iliyopita.

Uchafuzi wa hewa kutoka kwa viwanda unachangia katika kuongeza nyuzi joto.
Unsplash/Maxim Tolchinskiy
Uchafuzi wa hewa kutoka kwa viwanda unachangia katika kuongeza nyuzi joto.


Navyo vina vya maji baharini vimeongezeka kwa kasi kubwa tangu mwaka 1990, kuliko karne yoyote katika angalau miaka 3,000 iliyopita.Iwapo kiwango cha joto kitaendelea hivyo bila kudhibitiwa, itakuwa na madhara mabaya mno kwa binadamu, kwa ekoloji na kwa uchumi, na kusababisha uhaba wa chakula, majanga ya moto kuongezeka, kuongezaka kwa kina cha bahari na kusababisha hali mbaya mno ya hewa.

Fedha zilizopangwa kutolewa ili kusaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zimetolewa asilimia 21 pekee. Hivyo makampuni ya uwekezaji na mabenki yamehimizwa kuwekeza katika shughuli zinazolenga kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi angalau kwa asilimia 50 huku kipaumbele kikisisitizwa kutolewa kwa makundi yenye uhitaji zaidi ikiwemo wanawake na watoto.

Uzalishaji wa gesi ya ukaa usipopunguzwa kwa asilimia 7.6 kila mwaka kati ya 2020 na 2030, dunia haitaweza kufikia nyuzijoto 1.5 za kiwango cha joto zinazolengwa kufikiwa chini ya mkataba wa Paris

Wanawake wakishiriki kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi nchini Bangladesh
UNDP Bangladesh
Wanawake wakishiriki kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi nchini Bangladesh

 Nini suluhisho?

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa mapendekezo kadhaa ya kukabiliana na hali hii ambayo ni;- dunia kuhakikisha ina uchumi usioharibu mazingira na juhudi za makusudi kuhakikisha kuna hewa safi na nchi tajiri pamoja na mashirika makubwa ya kimataifa, kujiunga na umoja wa kutozalisha hewa ya kaboni. 

Pia amesisitiza kundi la nchi 20 zenye uchumi wa juu, au G20 zinatimiza ahadi zao kwa kutoa michango na kuweka sera zinazokubalika kimataifa kabla ya mkutano wa kimataifa wa masuala ya hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa unatarajiwa kufanyika huko Glasgow, Scotland baadaye mwaka huu 2021.

“Nchi za OECD lazima zimalize makaa ya mawe yaliyopo ifikapo mwaka 2030, na zingine zote zifuatazo ifikapo mwaka 2040. Nchi zinapaswa pia kumaliza utafutaji na uzalishaji mpya wa mafuta na kutafuta na kutoa ruzuku kwenye mafuta mbadala. Kufikia 2030, kuwe na uwekezaji mara nne zaidi kwenye umeme wa jua na upepo na uwekezaji wa nishati mbadala mara tatu zaidi.” amesema Guterres 

Utunzaji wa misitu, maeneo oevu, na mifumo mingine ya ekolojia ni muhimu katika kukabiliana na hali mbaya ya hewa, kutunza makazi, mimea, usambazaji wa maji na miundombinu. Kuhifadhi na kuboresha mifumo hii muhimu ya ekolojia kutasaidia kukabiliana na changamoto zilizopo hivi sasa katika sayari dunia.