Kasi ya ukatili wa kingono Somalia inatisha- UN

Umoja wa Mataifa unasema kumekuweko na ongezeko la kutisha la vitendo vya ukatili wa kingono nchini Somalia
© UNICEF/Kate Holt
Umoja wa Mataifa unasema kumekuweko na ongezeko la kutisha la vitendo vya ukatili wa kingono nchini Somalia

Kasi ya ukatili wa kingono Somalia inatisha- UN

Amani na Usalama

Ongezeko la kutisha la asilimia 80 la vitendo vya ukatili wa kingono nchini Somalia limewekwa bayana katika ripoti mbili za hivi karibuni za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambapo hii leo wawakilishi wake maalum wamesema ni jambo la kusikitisha.
 

Wawakilishi hao ni Virginia Gamba ambaye anahusika na watoto katika mizozo ya kivita na Pramila Patten ambaye ni mwakilishi katika masuala ya ukatili wa kingono vitani na wametoa maoni yao kupitia taarifa zao walizotoa wakitaka “pande zote kinzani nchini Somalia zikomeshe ukiukwaji huo.”

Wakimbizi wa ndani wanyanyasika

Ripoti za hivi karibuni kuhusu watoto kwenye mizozo ya kivita na ile ya ukatili wa kingono kwenye mizozo zimeonesha kuwa mwaka 2020 raia 400 wengi wao wakiwa watoto wa kike walikumbwa na vitendo vya ubakaji na aina nyingine za ukatili wa kingono.Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 80 ikilinganishwa na mwaka 2019.

Zaidi ya visa 100 vya ukatili wa kingono dhidi ya watoto wa kike vilithibitishwa na Umoja wa Mataifa katika robo ya kwanza ya mwaka 2021. Watekelezaji mara nyingi wanaonewa kutokana na hali ngumu zinazowakabili hasa watoto wa kike ambao huwa wamesalia kwenye kambi ili kutekeleza majukumu ya nyumbani.

Ukosefu wa usalama Somalia

Ripoti hiyo imeoanisha ukatili wa kingono na mazingira ya ukosefu wa usalama yaliyoshamiri nchini Somalia. Hali hiyo iliongezeka zaidi wakati wa mvutano wa kisiasa kuelekea uchaguzi wa kitaifa, mapigano ya kikabila kwa misingi ya kugombea maeneo na ongezeko la shughuli za kundi la Al Shabaab ambalo linasambaza misimamo mikali, vitendo hivyo vya Al Shabaab vimeshika kasi wakati huu wa janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19.

Halikadhalika, sitisho la muda la huduma za usalama na mahakama huku janga la Corona nalo likivuruga fursa za manusura wa ukatili wa kingono kupata huduma wanazohitaji.
Inaelezwa kuwa visa vya ukatili wa kingono vinavyohusishwa  na Al Shabaab vimeongezeka maradufu , ikibainisha jinsi kundi hilo la kigaidi linaendelea kutumia ukatili wa kingono na ndoa za lazima kuendelea kudhibiti maeneo ambayo wanashikilia kinyume cha sheria.

Manusura wa ubakaji akiwa katika kituo cha haki za wanawake mjini Mogadishu nchini Somalia akisimulia yaliyomsibu
UN Photo/Fardowsa Hussein
Manusura wa ubakaji akiwa katika kituo cha haki za wanawake mjini Mogadishu nchini Somalia akisimulia yaliyomsibu

Ukiukwaji wa haki unaotekelezwa na vikundi vya koo vilivyojihami nao umeongezeka mara tatu. Mambo yote hayo yamehusishwa na kuendelea kusambaa kwa silaha ndogo ndogo.
Katika matukio mengi, watekelezaji hawajatambuliwa kitendo ambacho kinazidi kuchochea watu kukwepa sheria.

Bi. Gamba na Bi. Patten wameeleza hofu yao kuwa zaidi ya asilimia 15 ya visa vya ukatili wa kingono vilivyothibitishwa, vimetekelezwa na vikosi vya usalama vya serikali.
Jeshi la ulinzi na lile la polisi nchini humo wametekeleza vitendo vya ubakaji na aina nyingine ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Hatua thabiti

Wawakilishi hao maalum wamesihi serikali ya Somali ichukue hatua thabiti kuzuia ukatili wa kingono dhidi ya wanawake na watoto.
Wameangazia umuhimu wa mpango wa utekelezaji wa mwaka 2021 wa kumaliza utumikishaji watoto jeshini na ratiba yam waka 2019 ambayo imeanzisha mfumo wa kuzuia ukatili wa kingono dhidi ya watoto.

Mpango wa  utekelezaji wa kitaifa

Halikadhalika wamesihi serikali iridhie haraka mpango mpya wa kitaifa wa kumaliza ukatili wa kingono kwenye mizozo.
Wamesema hatua hizo zitaimarisha sera ya kutovumilia kabisa ukatili wa kingono katika sekta ya ulinzi na usalama na kusaidia kuimarisha uwezo wa kitaasisi wa kuzuia kwa ufanisi na kuchukua hatua dhidi ya ukatili wa kingono.
Wabunge wa Somalia nao wametakiwa kuimarisha sheria ili kulinda vyema haki za wanawake na watoto. Wamegusia sera dhaifu ambazo zinapatia fursa kuwa huru huku manusura wakisalia na msaada kidogo au bila msaada kabisa.

“Mamlaka za Somalia lazima zitume ishara thabiti ya matumaini kwa manusura wa ukatili na ishara ya machukizo kwa watekelezaji wa vitendo hivyo au wanaopanga kufanya ukatili huo,” wamesema wawakilishi hao maalum wawili wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.