Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko China kwa kuchangia dozi milioni 500 za COVID-19: UN 

Chanjo
Janssen
Chanjo

Heko China kwa kuchangia dozi milioni 500 za COVID-19: UN 

Afya

China imetangaza kuwa inazalisha chanjo zaidi ya milioni 500 za Corona au COVID-19 kupitia kampuni mbili nchini humo, chanjo ambazo zitasambazwa kwa nchi maskini kupitia mfumo wa Umoja wa Mataifa, hatua ambayo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameipongeza kwa kuzingatia kuwa ni idadi ndogo tu ya watu katika nchi maskini ndio wamepatiwa chanjo ikiliinganishwa na zile za kipato cha juu.

Ndivyo inavyoanza video ya ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akisema janga la COVID-19 linaendelea kuangamiza ulimwengu wetu, na limesabaisha vifo vya zaidi ya watu milioni 4, ujumbe ambao  ameutoa kwenye jukwaa la kwanza la kimataifa la ushirikiano wa chanjo ya Corona lililofanyika nchini China. 

Guterres ameishukuru serikali ya China kwa uongozi wake kushughulikia upatikanaji sawa wa chanjo kwa nchi zinazoendelea. 

 “Ninakaribisha makubaliano yaliyosainiwa na Sinopharm na Sinovac na COVAX, ya usambazaji wa chanjo za Corona zaidi ya dozi milioni 500. Kwa jumla, dunia inahitaji dozi zaidi ya bilioni 11 ili kufanikisha kuchanja asilimia 70 ya idadi ya watu wote  ulimwenguni, ili hatimaye tuweze kuvuka kizingiti muhimu cha kufikia mwisho wa janga hili.” 

Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa chanjo hizo kufikia kila mtu, kila mahali na haraka iwezekanavyo na kutuma ombi maalum kwa nchi tajiri zaidi duniani. 

 “Dunia inahitaji mpango wa chanjo wa pamoja kwa ulimwengu ili angalau uzalishaji wa chanjo uongezeke mara mbili na kuhakikisha usambazaji sawa kupitia COVAX. Tunahitaji pia Kikosi Kazi cha Dharura kutoka kundi la nchi 20 tajiri au G20 ili  kuratibu utekelezaji wake.” 

Umoja wa Mataifa unasema mkutano huo wa kwanza wa jukwaa la kimataifa juu ya ushirikiano wa chanjo ya COVID-19 ni fursa muhimu ya kuleta pamoja nchi zilizo na uwezo wa uzalishaji wa chanjo, kampuni za dawa na wazalishaji, ili kuendeleza ushirikiano wa kimataifa juu ya chanjo.