Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sitisheni chanjo ya nyongeza dhidi ya COVID-19 hadi Septemba - WHO

Raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akipatiwa chanjo dhidi ya Corona au COVID-19 nchini humo.
© UNICEF/Arlette Bashizi
Raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akipatiwa chanjo dhidi ya Corona au COVID-19 nchini humo.

Sitisheni chanjo ya nyongeza dhidi ya COVID-19 hadi Septemba - WHO

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO limetaka sitisho la mpango wa baadhi ya nchi tajiri kutoa chanjo ya nyongeza kwa wananchi wao ili kukabiliana na awamu ya mnyumbuliko wa virusi vya ugonjwa wa Corona au COVID-19 aina ya Delta.

 

Wito huo umetolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi katika mikutano ya kila wiki ya mwelekeo wa ugonjwa wa Corona.

“WHO inatoa wito wa sitisho la chanjo ya nyongeza hadi angalau mwishoni mwa mwezi ujao wa Septemba ili kuwezesha angalau asilimia 10 wa wakazi katika kila nchi duniani iwe imepatiwa chanjo,” amesema Dkt. Tedros.

Amesema ili hili liwezekane, kunahitajika ushirikiano wa kila mtu, hususan nchi na kampuni chache ambazo zinadhibiti usambazaji wa chanjo duniani.

Kauli ya kutaka sitisho la chanjo ya nyongeza inakuja wakati ambapo kati ya zaidi ya chanjo bilioni 4 zilizosambazwa duniani, asilimia 80 zimetumika nchi tajiri ingawa idadi ya watu wao ni chini ya nusu ya idadi ya watu wote duniani.

“Natambua hofu ya serikali katika kulinda watu wake dhidi ya virusi vya coronavirus">COVID-19 aina ya Delta, lakini hatuwezi kukubali nchi ambazo tayari zimeshatumia kiasi kikubwa cha chanjo kutumia zaidi na zaidi huku wengi walio hatarini zaidi duniani hawajapata hata chanjo moja,” amesema Dkt. Tedros.

Kwa bara la Afrika hali ni mbaya zaidi kwa kuwa ni asilimia 1 tu ya wakazi wa bara hilo ndio wamepata chanjo dhidi ya COVID-19.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO ametoa wito kwa kundi la nchi tajiri duniani, au G20 kuchukua uamuzi wa busara mwezi ujao wakati wa mkutano wa mawaziri wao wa afya ili watimize ahadi ya kundi hilo ya  kufanikisha malengo ya WHO kuhusu utoaji wa chanjo ya COVID-19.