Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahisani wakutana kuchangisha fedha kunusuru Lebanon

Uharibifu katika Bandari ya  Beirut baada ya mlipuko mbaya zaidi mnamo 4 Agosti 2020.
© UNOCHA
Uharibifu katika Bandari ya Beirut baada ya mlipuko mbaya zaidi mnamo 4 Agosti 2020.

Wahisani wakutana kuchangisha fedha kunusuru Lebanon

Msaada wa Kibinadamu

Mkutano wa wahisani wenye lengo la kuchagiza kasi ya usaidizi kwa Lebanon, ikiwa ni mwaka mmoja tangu milipuko kwenye mji mkuu Beirut, ni fursa ya kipekee ya kuazimia upya ahadi kwa taifa hilo na kuzuia janga la kibinadamu, amesema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Matafa Amina J. Mohammed hii leo.

Mkutano huo wa kimataifa wa kusaidia wananchi wa Lebanon  umeitishwa na Ufaransa na Umoja wa Mataifa kwa lengo la kuchangisha dola milioni 350 na umefanyika hii leo ikiwa ni mwaka mmoja tangu milipuko katika bandari ya Beiruti isababishe vifo vya watu wapatao 200 huku wengine maelfu wamepoteza makazi.

“Miezi 12 sasa, fikra zetu zinasalia na familia za waliopoteza maisha pamoja na manusura na wale wengine wote walioathirika. Tunaendelea kusisitiza umuhimu wa uchunguzi huru na wa haki wa tukio hilo la mlipuko,” amesema Bi. Mohammed katika mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao.
Janga la kihistoria

Kwa sasa Lebanon inakabiliwa na moja ya majanga makubwa kuwahi kuikumba katika historia yake ya karibuni ambapo uchumi unatwama, hakuna utulivu wa kisiasa na wnanachi wanahitaji msaada kwa kuwa nusu ya wananchi wote ni fukara.

Halikadhalika nchi hiyo ni mwenyeji wa wakimbizi kutoka Syria na Palestina ambao pamoja na familia za wenyeji wa wahaiaji wanahitaij msaada wa dharura. Janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 nalo limezorotesha mifumo ya afya na kuathiri uchumi.

Mwanamke mmoja huko Beirut anatafuta mabaki nyumbani mwake baada ya mlipuko wa tarehe 4 Agosti kuporomosha nyumba yake.
© UNOCHA
Mwanamke mmoja huko Beirut anatafuta mabaki nyumbani mwake baada ya mlipuko wa tarehe 4 Agosti kuporomosha nyumba yake.

Kama hiyo haitoshi, kwa mwaka mzima sasa, Lebanon haina serikali. Naibu Katibu Mkuu akaeleza matumaini yake juu ya kuundwa haraka kwa serikali chini ya Waziri Mkuu Mteule Najib Mikati. 
“Wananchi wa Lebanon wana haki ya kuwa na taasisi imara ambazo zinaweza kuwapatia misaada, haki na kushughulikia changamoto. Na serikali ya maslahi ya taifa inaweza kusongesha marekebisho na utulivu, ukuaji uchumi sambamba na kutoa fursa ya demokrasia na fursa za kuchechemua uwezo wa vijana wa kike na wa kiume wa Lebanon,” amesema Bi. Mohammed.

Kuna mengi zaidi ya kufanya

Bi. Mohammed ametaja jinsi Umoja w Mataifa na wadau wamesaidia Lebanon baada ya janga la milipuko ikiwemo kujenga upya mifumo ya kusambaza maji, sambamba na kukarabati shule na hospitali.
Amewaambia wahisani kuwa iwapo kuna ufadhili zaidi unapatikana, basi mambo mengi zaidi yanaweza kufanyika.

“Hii leo tuna fursa ya kipekee ya kutangaza upya ahadi yet una kutoa msaada wa fedha unaohitajika kusaidia watu wa Lebanon na kuzuia janga zadi la kibinadamu.”
Hata hivyo amesema hatua za dharura hazitakuwa suluhu ya kudumu, badala yake kinachohitajika ni mifumo ya kujikwamua kwa muda mrefu zaidi kwa kuzingatia malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Mazingira yanayohitajika

Mifumo thabiti, jumuishi nay a kina kuhusu hifadhi ya jamii hususan inayolenga kusaidia watu walio hatarini zaidi.

“Tunahitaji mazingira rafiki ya kusongesha hali ya sasa- na hatimaye Lebanon inahitaji serikali iliyojiandaa kutekeleza marekebisho ya haraka,” amesema Bi. Mohammed.