Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Roboti uwanja wa Jomo Kenyatta zapima COVID-19 na kufukiza dawa 

Uwezo bandia unafungua milango katika kuboresha huduma ya afya ulimwenguni.
Unsplash/Possessed Photography
Uwezo bandia unafungua milango katika kuboresha huduma ya afya ulimwenguni.

Roboti uwanja wa Jomo Kenyatta zapima COVID-19 na kufukiza dawa 

Afya

Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP nchini Kenya linaendesha programu ya majaribio ya kutumia roboti katika kupima afya za wasafiri wanaoingia na kutoka katika uwanja wa ndege wa kimataifa Jomo Kenyatta jijini Nairobi pamoja na Hospitali Kuu ya Taifa ya Kenyatta lengo likiwa ni kuongeza ufanisi na kuwapunguzia mzigo watendaji wa sekta ya afya.

Eneo ni uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta, jijini Nairobi nchini Kenya, video ya Shirika la mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP inaonesha roboti tatu zikiwa zimefungwa vifaa viwili vinavyomwaga dawa ya kuua vijidudu, kupima  joto la mwili, kufuatilia, kutunza taarifa za abiria pamoja na usimamizi wa wagonjwa.   

 Mwakilishi mkazi wa UNDP nchini Kenya Walid Badawi anasema majina ya roboti hizo tatu ni  Jasiri, Tumaini na Shujaa.  

 “Mwanzoni mwa janga hili la Corona UNDP tulitoa fursa ya kusaidia ulimwengu kulingana na maono yetu kama shirika la maendeleo katika maeneo ya kujiandaa, kukabiliana na kupona changamoto zilizoletwa na janga hili” 

 Watendaji kadhaaa katika uwanja huu na halikadhalika Hospitali Kuu ya Kenyatta wamepatiwa mafunzo ambapo Dkt Amina Guleid ni mwenyekiti wa kamati ya kusimamia programu hii ya roboti na  anasema, “mpaka sasa tumeshawafundisha wataalamu wetu watano wa TEHAMA namna ya uendeshaji wa roboti hizi, na tunaendelea na watoa huduma wengine wa afya, na madaktari ambao watatoa ushauri wa kitaalamu kwenye masuala ya kliniki. Lakini pia tunaye mtaalamu wa afya ambaye anahusika kwenye eneo la kufukiza dawa na ndio anatuongoza namna sahihi ya kufukiza.” 

 Roboti hizo pia zinaepusha wahudumu wa afya kuwa karibu na abiria na hivyo kupunguza hatari ya kupata maambukizi ya Corona. 

Utaalamu huu wa kutumia roboti umebuniwa na kampuni ya Zorabots Afrika Limited chini ya ufadhili wa UNDP Rwanda, na Mkurugenzi mtendaji wake Benjamin Kerenzi anasema zina uwezo wa kuchakata takwimu na kutoa taarifa wakati huo huo, hivyo kuwasaidia wafanya maamuzi kuwa na taarifa sahihi.