Watu 700 wamekufa katika mashambulizi kwenye vituo vya afya

3 Agosti 2021

Zaidi ya wafanyakazi wa afya 700 na wagonjwa wamekufa, na wengine zaidi ya 2000 walijeruhiwa katika mashambulizi yaliyofanywa kwenye vituo vya afya tangu mwaka 2017.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya miaka mitatu iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO.
 
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hii leo, Mkurugenzi wa Afya na Huduma za Dharura , WHO, Altaf Musani amesema “tuna wasiwasi mkubwa kwamba mamia ya vituo vya afya vimeharibiwa au kufungwa, wahudumu wa afya waliuawa au kujeruhiwa, na mamilioni ya watu walinyimwa huduma ya afya inayostahili”.
 
Ripoti hiyo ya ufuatiliaji wa mashambulizi ya huduma za afya kuanzia mwaka 2018 mpaka 2020 imerekodi takwimu za kushambuliwa watoa huduma za afya, wagonjwa, vifaa, magari ya kubebea wagonjwa na vituo katika nchi 17 vimeathirika na vipo katika mazingira dhaifu.
Nchi hizo ni pamoja na Ethiopia, Yemen, Syria, Msumbiji, Nigeria, Palestina, Myanmar, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Somalia.
 
Akitoa undani zaidi wa utafiti huo Musani amesema “katika kila tukio moja kati ya sita, yamegharimu maisha ya watoa huduma za afya mwaka 2020, watoa huduma ndio waathirika wakubwa, wakiwakilisha theluthi mbili ya mashambulizi yote ya mwaka 2018, 2019 na asilimia hamsini ya matukio yaliyorekodiwa mwaka 2020 ikilinganishwa na vifaa na vituo vya afya.”
 
Mkurugenzi huyo wa WHO amezipata pande zote zinazokuwa kwenye mizozo kuzingatia umuhimu wa watoa huduma na vituo vya afya kwani kila tukio lina madhara ya muda mrefu hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anawalinda watoa huduma na maeneo ya kutolea huduma za afya.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter