Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Milipuko Beirut yatimu mwaka mmoja, familia asilimia 98 bado zahitaji msaada

UNDP imekuwa ikunga mkono juhudi za ukarabati ikiwemo kuweka paneli za nishati ya jua.
UNDP Lebanon
UNDP imekuwa ikunga mkono juhudi za ukarabati ikiwemo kuweka paneli za nishati ya jua.

Milipuko Beirut yatimu mwaka mmoja, familia asilimia 98 bado zahitaji msaada

Amani na Usalama

Mwaka mmoja tangu kutokea kwa milipuko kwenye mji mkuu wa Beirut, Lebanon, mahitaij ya watoto na familia zao yamesalia kuwa makubwa yakichochewa zaidi na kuporomoka kwa uchumi, ukosefu wa utulivu wa kisiasa na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19. 

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na kutolewa leo Agosti tatu mjini Beirut. 

Tathmini hiyo inaonesha watoto kukumbwa na kiwewe sambamba mahitaji ya msingi yanayokabili familia zao. 

Kaya 7 kati ya 10 ziliomba misaada ya msingi tangu tarehe 4 mwezi Agoti mwaka jana na takribani kaya zote hizo hadi leo zinategemea misaada ya kibinadamu kama vile fedha kwa ajili ya kununua chakula. 

Theluthi moja ya familia zenye watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 zimesema angalau mtoto mmoja katika familia alikuwa na dalili za kiwewe na msongo wa mawazo huku kwa watu wazima takribani nusu yao wanakumbwa na hali hiyo. 

Mwakilishi wa UNICEF nchini Lebanon Yukie Mokuo anasema, “mwaka mmoja baada ya tukio lile la kutisha na kusikitisha, maisha ya watoto bado yameathirika. Hicho ndicho wazazi wao wanatueleza.. Familia zinahaha kupona baada ya milipuko ile mibaya zaidi kuwahi kutokea tena katikati ya janga la kiuchumi na kiafya.” 

Milipuko hiyo ilisambarataisha eneo kubwa la mji wa Beirut na kuua zaidi ya watu 200 wakiwemo watoto huku majeruhi walikuwa zaidi ya 6,500 na wakiwemo watoto 1,000. 

Kwa kuwa biashara zilisambaratishwa, makumi ya maelfu ya wafanyakazi walipoteza ajira na kuwaacha wakihaha kulisha familia zao na kutibu watoto. 

Utafiti huo wa UNICEF unasema familia mbili kati ya tatu sawa na asilimia 68.6 hazijaweza kupata huduma za afya tangu mlipuko kutokea. 

UTafiti huo unatokana na mahojiano kwa njia ya simu yaliyofanyika mwezi uliopita wa Julai na kuhusisha kaya 1,187. 

Kwa mantiki hiyo UNICEF inatoa wito wa mambo kadhaa ikiwemo watoto kupatiwa kipaumbele na hazi zao za msingi ziheshimiwe. Pili viongozi wa kisiasa Lebanon wamalize tofauti zao na kuunda serikali ya kuhudumia wananchi. Tatu mamlaka zitambue kuwa kuendeleza huduma za umma kwa muda mfupi na mrefu ni muhimu kwa uhai na maendeleo ya mtoto.