Unyonyeshe vipi mtoto wakati wa COVID-19? Pata Mwongozo wa UNICEF

2 Agosti 2021

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limetoa mwongozo wa unyonyeshaji mtoto salama wakati huu dunia inakabiliana na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 na kutoa maelekezo ya kumlisha mtoto kwa kufuata mwongozo huo.

Kama ni mama au mjamzito anategemea kujifungua siku za karibuni ni kawaida kuwa na maswali iwapo ni salama kwa mtoto kunyonyeshwa katika kipindi hiki cha janga la Corona.

Ushahidi mkubwa unaunga mkono unyonyeshaji mtoto maziwa ya mama. Maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto hayajaonekana katika tafiti zilizofanyika. Badala yake unyonyeshaji mtoto na mama na mtoto kugusana ngozi wakati wa unyonyeshaji vimeonekana kuwa na manufaa zaidi kwa mtoto kwani humsaidia mtoto kustawi pamoja na faida nyinge za kiafya na maisha.

Yafuatayo ni majibu ambayo wataalamu wamefafanua kutokana na maswali mengi yaliyoulizwa na wanawake wanao nyonyesha pamoja na wajawazito ambao watarajia kuanza kunyonyesha karibuni.

Ninyonyeshe kipindi cha janga la Corona?

Ndio, hakuna ushahidi mpaka leo ulioonesha mtoto ameambukizwa COVID-19 kutokana na kunyonya maziwa ya mama.

Mtoto mwenye umri wa chini ya miezi 6 anapaswa kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee. Baada ya kufika miezi sita ataendeelea kunyonyeshwa na kupewa vyakula salama na vyenye afya.

Maziwa ya mama yanatoa kingamwili zinazowapa watoto nguvu ya afya na kuwalinda dhidi ya maambukizo mengi. Kunyonyesha kunapunguza sana hatari ya kifo kwa watoto waliozaliwa na watoto wachanga, pia unyonyeshaji unaboresha afya ya mama.

Mama anapogusana ngozi kwa ngozi na mtoto wake mchanga, anapomuweka mtoto karibu husaidia kuanza mapema kwa kunyonyesha. Muda sahihi wa kuanza unyonyeshaji ni ndani ya saa ya kwanza baada ya kujifungua.

.

Lucy Atokoru, 28 ananyonyesha mtoto wake nyumbani kwake Omugo, Wilaya ya Arua.
© UNICEF/Zahara Abdul
Lucy Atokoru, 28 ananyonyesha mtoto wake nyumbani kwake Omugo, Wilaya ya Arua.

 Unaweza muambukiza mtoto COVID-19 kwa kunyonyesha?

Mpaka sasa virusi vya COVID-19 havijaonekana katika maziwa ya mama yeyote aliyegundulika kuugua ugonjwa huo anayenyonyesha, kwa hivyo haiwezekani kwamba COVID-19 inaweza kupitishwa kupitia maziwa ya mama.
Watafiti bado wanaendelea kupima maziwa ya mama kutoka kwa mama aliyebainika au anayehisiwa kuwa na COVID-19.

Niendelee kunyonyesha iwapo nimeshukiwa au kubainika na COVID-19?

Ndio, unatakiwa kuendelea na unyonyeshaji huku ukizingatia mwongozo wa kujikinga na Corona. Utafiti uliofanyika mpaka sasa haujagundua uwepo wa maambukizi ya COVID-19 kupitia maziwa ya mama na unyonyeshaji.
Uvaaji wa barakoa, kunawa mikono na sabuni na maji tiririka kabla na baada ya kumshika mtoto , usafi wa mara kwa mara wa mazingira kuua vijinunu unaendelea kumiziwa. Kifua cha mama kinatakiwa kusafishwa iwapo tuu amekoholea eneo hilo, ziwa la mama halihitajiki kusafishwa kila anapotaka kunyonyesha mtoto.

Ninaweza kupata chanjo ya Corona wakati nanyonyesha?

Ndio, wataalamu wa afya wanahimiza wakina mama wanao nyonyesha au kukamua maziwa kupata chanjo ya COVID-19 
 

Mama akimnyonyesha mtoto wake huko Mongolia
UNICEF/Ilvy Njiokiktjien VII Photo
Mama akimnyonyesha mtoto wake huko Mongolia

 Ni salama kuendelea na unyonyeshaji baada ya kupata chanjo?

Ndio, ni salama kuendelea kunyonyesha mtoto baada ya kupata chanjo ili kuendela kumlinda mtoto.
 Hakuna chanjo yoyote iliyothibitishwa na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO ambayo inatumika yenye virusi hai, kwa hiyo hakuna hatari ya kusambaza virusi kupitia unyonyeshaji.

Nifanye nini iwapo nitajisikia kuumwa na kushindwa kunyonyesha?

Kama unajisikia kuugua na kushindwa kunyonyesha mtoto, jaribu kutafuta njia mbadala za kuhakikisha mtoto anapata maziwa ya mama. Jaribu kukamua maziwa na kumpa mtoto kwakutumia kikombe kisafi. Pia unaweza kufikiria mtoto wako kunyonyeshwa na mama mwingine iwapo yupo katika eneo hilo.

Zungumza na mshauri wa unyonyeshaji au mtaalamu katika kituo cha afya ili muweze kuangalia njia mbalimbali mnazoweza kutumia iwapo utashindwa kumnyonyesha mtoto.

Kukamua maziwa ni hatua nzuri ya kukusaidia kuendelea na unyonyeshaji baada ya afya yako kurejea vizuri. Hakuna muda maalum umewekwa wa kuanza kunyonyesha baada ya kutoka kuugua COVID-19.

Iwapo hakutakuwa na fursa ya mtu mwingine kumnyonyesha mtoto, hapo unaweza kufikira pia kunyonyesha kwa muda maziwa mbadala ya kopo lakini ni muhimu kuzingatia vipimo na usafi wakati wa uandaaji wa maziwa hayo .
 

Hellen Talemwa, mkazi wa Uganda akiwa na mwanae. Anasema COVID-19 inakwamisha mipango yake ya kumnyonyesha mwanae maziwa ya mama.
UN/ John Kibego
Hellen Talemwa, mkazi wa Uganda akiwa na mwanae. Anasema COVID-19 inakwamisha mipango yake ya kumnyonyesha mwanae maziwa ya mama.

 Naweza kuendelea kunyonyesha mtoto wangu iwapo anaumwa?

Endelea kumnyonyesha mtoto hata kama anaumwa. Iwapo mtoto wake amepata COVD-19 au ungonjwa mwingine wowote, nimuhimu kuendelea kumpa afya kupitia maziwa anayo nyonya, hii itamsaidia kupambana na maambukizi yanayomkabili.

Tahadhari gani ninapaswa kuchukua wakati wa kunyonyesha?

Hakikisha unafuata miongozo ya kunawa mikono. Mikono yako inatakiwa kusafishwa na sabuni na maji tiririka kabla na baada ya kumshika mtoto. Unaweza pia tumia vitakasa mikono. Ni muhimu pia kusafisha maeneo ambayo umeshika.

Safisha mashine ya kukamulia maziwa, chupa za kuhifadhia maziwa na chuchu za chupa za kumnyonyeshea mtoto kila baada ya kuzitumia.
 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter