Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanaotegemea msaada wa kibinadamu wana hali tete

Watu milioni mbili na nusu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ( CAR)wanakabiliwa na njaa
WFP/Bruno Djoye
Watu milioni mbili na nusu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ( CAR)wanakabiliwa na njaa

Wanaotegemea msaada wa kibinadamu wana hali tete

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa lile la chakula na kilimo FAO na la mpango wa Chakula duniani WFP yameeleza jitihada za kupambana na kuongezeka kwa ukosefu wa usalama wa chakula zinazofanyika katika nchi kadhaa zinashindikana kutokana na kuwepo kwa mapigano na vizuizi ambavyo vimekwamisha ufikishaji misaada ya kuokoa maisha ya familia zinazokabiliwa na njaa. 

Taarifa iliyotolewa leo Roma nchini Italia na mashirika hayo mawili imesema vikwazo vitokavyo na urasimu, mizozo, janga la Corona, pamoja na ukosefu wa fedha pia vimechangia kukwamisha juhudi za mashirika hayo kutoa msaada wa dharura wa chakula na kuwezesha wakulima kupanda kwa kiwango na kwa wakati unaofaa

Mkurugenzi mkuu wa FAO Qu Dongyu amesema “watu wengi walio hatarini ni wakulima. Pamoja na msaada wa chakula, lazima tufanye kila liwezekanao ili kuwasadia kuanza tena uzalishaji wa chakula wenyewe, ili familia zao ziweze kurejea katika kuzalisha chakula cha kujitosheleza na sio kutegema misaada ili kuishi”

Hata hivyo amebainisha kuwa suala hilo litakuwa gumu kufikiwa na wakulima bila ya kuwepo kwa fedha za kutosha kwakuwa mpaka sasa suala la msaada kwenye kilimo unategemea zaidi wafadhili, na kwa namna ilivyo sasa haiwezi kuepukika hivyo wafadhili wanaombwa kuchangia fedha. 

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa WFP David Beasley amesema wanaotegemea msaada wa kibinadamu wana hali tete. “Familia ambaz zinategemea misaada ya kibandamu kuishi zinaning;inia kwenye uzi. Wakati hatuwezi kuwafikia uzi wao hukatika, matokeo yake ni maafa”

Mfanyakazi akitoa chakula cha msaada katika ghala la WFP huko Sana'a
WFP/Mohammed Awadh
Mfanyakazi akitoa chakula cha msaada katika ghala la WFP huko Sana'a

   Nchi zenye hali mbaya zaidi 

Mashirika hayo yameeleza wasiwasi wao unazidi kuongezeka kutokana na kuendelea kwa mizozo, athari za kiuchumi zilizo sababishwa na janga la COVID-19 pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa ambapo wameeleza ndani ya miezi minne 4 ijayo ukosefu wa vyakula utakuwa wa hali ya juu zaidi katika maeneo takribani 23.

Nchi hizo 23 zilizo hatarini zaidi ni Afghanistan, Angola, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sahel ya Kati, Chad, Colombia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ethiopia, El Salvador, Honduras, Guatemala, Haiti, Kenya, Lebanon, Madagascar, Msumbiji, Myanmar, Nigeria, Sierra Leone, Liberia, Somalia, Sudan Kusini, Syria na Yemen.