Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufugaji wa Samaki kwenye mapipa nchini Cameroon

FAO imetoa mafunzo ya kilimo kwa wakimbizi wa ndani wanaume na wanawake ili waweze kufuga samaki kwa ajili ya kujipatia kitoweo na kipato cha ziada
© FAO Cameroon
FAO imetoa mafunzo ya kilimo kwa wakimbizi wa ndani wanaume na wanawake ili waweze kufuga samaki kwa ajili ya kujipatia kitoweo na kipato cha ziada

Ufugaji wa Samaki kwenye mapipa nchini Cameroon

Ukuaji wa Kiuchumi

Wakimbizi wa ndani nchini Cameroon wamegeukia ufugaji samaki kwakutumia mapipa katika kujitafutia kipato ili kuweza kujikimu.

Wakimbizi wa ndani raia wa Cameroon ambao wameyakimbia makazi yao kutokana na mizozo na mabadiliko ya tabianchi katika nchi hiyo iliyopo kaskazini mwa Afrrika Magharibi wamegeukia ufugaji wa samaki ikiwa ndio njia mbadala ya kuwapatia kipato baada ya kupatiwa mafunzo na shirika la Umoja wa mataifa la chakula na kilimo FAO.

Wakimbizi hao wamekuwa wakijifunza namna ya ufugaji wa samaki kwakutumia mapipa katika maeneo ambayo utamaduni wao wa kilimo ni kufuga mifugo, kulima na kuvua Samaki katika ziwa Chad.

Wakimbizi wa ndani wamepatiwa mafunzo ya kuwaandaa samaki kwa ajili ya kwenda kuwauza
© FAO Cameroon
Wakimbizi wa ndani wamepatiwa mafunzo ya kuwaandaa samaki kwa ajili ya kwenda kuwauza

Kuna zaidi ya wakimbizi wa ndani 300,000 kaskazini mwa nchi ya Cameroon ambao wamefurushwa kwenye makazi yao kutokana na mizozo na kupungua kina cha maji cha ziwa Chad kutokana na mabadiliko ya tabianchi. 

Mwanzoni mwa mwaka 2021, watu milioni 2.7 ndio walizaniwa watakuwa na tatizo la njaa katika nchi hiyo, lakini janga la Corona au COVID-19 limezidisha baa la njaa kwa idadi kubwa zaidi ya watu.