Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sauti za waathirika wa usafishirishaji haramu wa binadamu ziwe msingi wa mapambano - UN 

Msichana wa miaka minane anaficha uso wake katika kituo kinachoungwa mkono na UNICEF ambacho hutoa huduma ya muda na usaidizi kwa watoto waliosafirishwa kiharamu huku mamlaka zikiwatafuta wazazi wao nchini Haiti.
UNICEF/Marco Dormino Msichana wa umri wa miaka nane akiwa kwenye kituo cha kuhudumia watoto waliosafirishwa kwa njia haramu akiwa Haiti.

Sauti za waathirika wa usafishirishaji haramu wa binadamu ziwe msingi wa mapambano - UN 

Haki za binadamu

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kupinga usafirishaji haramu binadamu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake mahususi kwa ajili ya siku hii, ametoa wito kwa ulimwengu kuhakikisha wanawahusisha manusura na maathirika wa matukio ya usafirishaji haramu wa binadamu katika vita dhidi ya matendo hayo.

Guterres amesema, “katikati ya janga la ulimwengu, likiambatana na kuongezeka kwa ukosefu wa usawa na uharibifu wa uchumi, sauti za manusura na waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu ziko hatarini kuzamishwa. Lakini kusikiliza masimulizi yao ni muhimu zaidi kuliko wakati wowote kwani mgogoro wa coronavirus">COVID-19 unaongeza udhaifu na husababisha wasiwasi.” 

Watu kufikia milioni 124 zaidi wamesukumwa katika umaskini uliokithiri kutokana na janga la Covid-19, na kuwaacha mamilioni wengi wakiwa katika hatari ya kusafirishwa kiharamu. 

“Watoto wako katika hatari kubwa na inayoongezeka, wanawakilisha theluthi moja ya waathiriwa ulimwenguni, hali ambayo imeongezeka mara tatu katika miaka 15 iliyopita. Nusu ya waathirika katika nchi zenye kipato cha chini ni watoto, ambao wengi wao husafirishwa kwenda kufanyishwa kazi za kulazimishwa”, amesema Guterres akiongeza kuwa, “wahalifu kila mahali wanatumia teknolojia kutambua, kudhibiti na kuwanyonya watu walio katika mazingira magumu. Watoto wanazidi kulengwa kupitia majukwaa mtandaoni ya unyonyaji wa kijinsia, ndoa za kulazimishwa na aina zingine za unyanyasaji.” 

Usafirishaji haramu wa wanawake na wasichana kwa madhumuni ya unyanyasaji wa kijinsia unaendelea kuwa moja ya aina ya biashara zilizoenea zaidi na za kuchukiza. Wahamiaji wakiwa ndio idadi kubwa zaidi ya nusu ya wale wanaouzwa katika maeneo mengi. 

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa akaitumia siku hii kupeleka ujumbe kwa serikali ulimwenguni akisema, “ni lazima zichukue hatua za dharura kuimarisha kinga, kusaidia waathirika na kuwafikisha wahusika mahakamani. Hii ni pamoja na utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Uhalifu wa Kupangwa wa Kitaifa na Itifaki yake ya Kuzuia, Kukandamiza na Kuadhibu Usafirishaji Haramu wa Watu.” 

Mvulana mwenye huzuni anaonyeshwa katika kolagi ya kisanii, huku mkono wake ukifunika uso wake na kuzungukwa na rangi za kung'aa na mifumo ya nukta.
UNODC Usafirishaji haramu unapingwa na Umoja wa Mataifa.

Guterres ameendelea kueleza akisema jitihada za ulimwengu lazima ziongozwe na manusura wa usafirishaji haramu. Mchango wao ni muhimu kushughulikia mambo ya hatari na mifumo, na kutambua na kulinda waathirika na kuhakikisha ufikiaji wao wa haki na kupona, huku wakiwajibisha wanyonyaji wao. 

Umoja wa Mataifa umejitolea kusikiliza na kujibu sauti za waathirika na manusura wa biashara haramu ya binadamu, kuhakikisha haki zao na utu, kukuza simulizi zao zao na kujifunza kutoka kwao katika vita vyetu vya kuzuia na kumaliza uhalifu huu mbaya. 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Madawa na Uhalifu, UNODC, Ghada Waly kupitia ujumbe wake kuhusu siku hii alioutoa leo Julai 30 mjini Vienna, Austria amesema, kila mmoja wa waathirika wa usafirishaji haramu wa watu ana simulizi inayopaswa kusikilizwa. 

“Sauti za wahanga ni ufunguo wa kuzuia usafirishaji, kusaidia waathirika, na kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria. Wafanyabiashara huchagua waathirika wao kati ya walio katika mazingira magumu, wakitumia unyonge na ukosefu wa ufahamu. Wengi wa wale wanaolengwa ni watu wenye mahitaji ya kiuchumi ambao wanapotoshwa.” Amesema Ghada Waly. 

Nukuu ya Ghada Waly, Mkurugenzi Mtendaji wa UNODC, kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu, na picha yake mbele ya bendera UN .

Akifafanua takwimu, Waly amesema, “karibu theluthi mbili ya waathirika wanaogunduliwa ni wanawake na wasichana, na idadi ya watoto imeongezeka mara tatu katika miaka 15 iliyopita. Lakini licha ya udhaifu wao wa kweli na dhahiri, waathirika wa usafirishaji haramu ni mifano ya nguvu, ujasiri, na uthabiti.” 

Aidha Bi Waly akaitumia siku hii kuongea na maathirika wa matukio haya akisema, “katika Siku hii ya kupambana dhidi ya ya Usafirishaji haramu wa Binadamu, nawasalimu waathirika wote wanapojenga upya maisha yao na kusaidia kulinda maisha ya wengine.” 

UNODC imezindua kampeni inayoitwa Sauti za 'Waathirika' Ziongoze Njia' ili kuweka angalizo kwa hadithi zisizoelezeka za wahanga, na majukumu yao katika vita dhidi ya usafirishaji haramu. Nchi Wanachama lazima zishiriki, zisikilize, na kujifunza kutoka kwa manusura, na zisaidie mashirika yanayoongozwa na waathirika.