Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchango wa UNICEF katika sekta ya afya Zambia umeleta mabadiliko chanya katika jamii

Mtoto Blessing, mwenye umri wa miaka minne huenda na mama yake katika kliniki ya chanjo iliyoanzishwa na UNICEF kwenye viunga vya mji mkuu wa Zambia, Lusaka.
© UNICEF/Karin Schermbrucker
Mtoto Blessing, mwenye umri wa miaka minne huenda na mama yake katika kliniki ya chanjo iliyoanzishwa na UNICEF kwenye viunga vya mji mkuu wa Zambia, Lusaka.

Mchango wa UNICEF katika sekta ya afya Zambia umeleta mabadiliko chanya katika jamii

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limekuwa msaada mkubwa katika sekta ya afya nchini Zambia wakati wa ugonjwa wa Covid-19 nchini Zambia na hata kabla ya janga hili kuikumba dunia.
 

Daktari Rogers Mwale, Mtaalamu wa afya wa UNICEF nchini Zambia akitukaribisha katika kliniki ya mji eneo la  George kwenye viunga vya mji mkuu wa Zambia, Lusaka. Daktari huyu anasema eneo hili ni moja ya maeneo yenye msongamano wa watu nchini hapa. UNICEF imekuwa ikifanya shughuli zake hapa kuisaidia wizara ya afya ya Zambia kutoa huduma za afya kwa wanawake na watoto ili kuwahakikishia watoto wanakuwa na mwanzo mzuri katika maisha.  

Bridget Banda ni muhudumu wa afya katika kituo hiki cha afya cha George anasema, “tumeona matokeo kweli, jamii yetu inafaidika na hii huduma na kuzalisha kwetu kumeongezeka. Hivi sasa tunaweza kusaidia wanawake takribani  mia nne na kitu hivi kwa mwezi.” 
UNICEF imeboresha miundombinu katika vituo hivi vya afya vya Lusaka na Copper Belt ambapo wameboersha mitambo ya maji, vifaa, ujuzi wa wafanyakazi na hali ya jumla ya vituo hivi na matokeo yamekuwa chanya.

Lenny Mukupa mnufaika wa mabadiliko haya na sasa amekibeba kichanga chake baada ya kujifungua hivi karibuni. Hapa anakumbuka hali ilivyokuwa kabla ya msaada kutoka UNICEF, “Mara ya mwisho nililazwa hapa miaka mitano iliyopita. Sasa ninaweza kuona tofauti kati ya wodi ya zamani na sasa. Kipindi chan yuma nafasi kati ya kitanda na kitanda ilikuwa haitoshi. Tulikuwa tunalazimika kuweka matandiko yetu sakafuni . Vyoo havikuwa visafi. Tofauti nyingine niliyoiona, katika wodi za zamani nisingweza kukaa muda mrefu baada ya kujifungua. Nilijifunua saa kumi na mbili asuBuhi nikaruhusiwa saa nne asubuhi kwa kuwa nafasi ilikuwa haitoshi. Lakini wakati huu nimejifungua jana saa kumi na mbili dakika arobaini jioni na bado nipo kusubiri wauguzi wafuatilie afya yangu mimi na mtoto.Ninaishukuru serikali na UNICEF kwa kuboresha hodi ya wazazi. ” 

Muhudumu wa afya Briget  anarejea akisema, “kimsingi huduma zote ni bila malipo na kwamba wanajisikia vizuri kufanya kazi katika mazingira kama haya kwa sababu yanawahamasisha kufanya kazi na kuwahudumia wanawake kwa sababu kabla ulikuwa unalamika kuungaunga vitu vya kutumia lakini hivi sasa tuna vifaa, tuna maarifa. Kwa hivyo unahamasika kufanya kazi kwa sababu una unavyovihitaji kufanya kazi, unafanya kazi katika mazingira safi na unaweza kuelewana vizuri na wanake.”