Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yapatia maafisa na askari wa jeshi la DRC pamoja na polisi mbinu za medani  

Jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, maafisa wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani, MONUSCO wakipatia vyeti maafisa na askari wa jeshi la taifa, FARDC na jeshi la polisi waliopata mafunzo ya mwezi mmoja ya mbinu za medani.
MONUSCO
Jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, maafisa wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani, MONUSCO wakipatia vyeti maafisa na askari wa jeshi la taifa, FARDC na jeshi la polisi waliopata mafunzo ya mwezi mmoja ya mbinu za medani.

MONUSCO yapatia maafisa na askari wa jeshi la DRC pamoja na polisi mbinu za medani  

Amani na Usalama

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani, MONUSCO umepatia mafunzo ya mbinu za medani na usimamizi wa vilipuzi sambamba na ufyatuaji wa risasi, maafisa na wanajeshi 652 wa vikosi vya jeshi la serikali, FARDC na jeshi la polisi kama njia mojawapo ya kuimarisha ulinzi nchini humo.

Mafunzo hayo ya kuanzia tarehe 9 hadi 23 ya mwezi huu wa Julai, yamefanyika kinadharia na kivitendo katika kambi za Rwampara na Ndoromo zilizoko jimboni Ituri nchini DRC. 

Walinda amani wa Umoja waMataifa kutoka Guatemala wakisaidiwa na vikosi kutoka Bangladeshi na Nepal waliendesha mafunzo hayo ambayo pia yalihusisha kuongeza uelewa kuhusu haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu pamoja na ulinzi wa wakimbizi wa ndani na ukatili wa kingono vitani. 

MONUSCO imeendesha mafunzo hayo kama sehemu ya  majukumu yake ya kujengea uwezo vikosi vya ulinzi na usalama DRC ili viweze kutekeleza vyema majukumu ya ulinzi wa raia. 

Bertin Ory ambaye ni Mkuu wa ofisi ya pamoja ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa na DRC  mjini Bunia jimboni Ituri amesema “mafunzo haya yamelenga maafisa wa jeshi, kwa sababu wao ndio wanapaswa kuonesha ni maeneo gani hawapaswi kuvuka wakati wa operesheni zao, mathalani kuheshimu haki za binadamu, utu wa kibinadamu, na sheria za kimataifa za kibinadamu. Tumeridhika kwa sababu wameahidi kufikisha ujumbe kwa vikosi vyao.” 

MONUSCO pia imesisiiza ahadi yake ya kusaidia jeshi la DRC msaada unaotakiwa kutokomeza vikundi vilivyojihami huko Ituri kama ilivyopendekezwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. 

“Ninyi ndio mtashinda hii vita. Ninyi ndio mtatokomeza hivi vikundi vilivyojihami,” amesema Luteni Jenerali Marcos De Sá Affonso Da Costa ambaye kamanda wa MONUSCO. 

Wanajeshi hao wa MONUSCO sasa watasambazwa katika maeneo mbalimbali kama sehemu ya operesheni ya hali ya hatari iliyotangazwa jimboni Ituri ambako vikundi vilivyojihami vya ndan na nje ya DRC vinaendeleza mashambulizi dhidi ya raia.