Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Anayepinga Corona aulize koo zilizokumbwa na janga- Rais Samia

Rais wa Tanzania akipokea chanjo dhidi ya COVID-19.
Ikulu Tanzania
Rais wa Tanzania akipokea chanjo dhidi ya COVID-19.

Anayepinga Corona aulize koo zilizokumbwa na janga- Rais Samia

Afya

Hii leo huko nchini Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan amezindua kazi ya utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Corona au COVID-19 kwa yeye mwenyewe kupatiwa chanjo hiyo pamoja na viongozi wengine waandamizi wa serikali, huku akisisitiza juu ya usalama wa chanjo hiyo  iliyowasili nchini humo mwishoni mwa wiki kupitia mpango wa Umoja wa Mataifa wa kusaka chanjo, COVAX.

Uzinduzi huo umefanyika Ikulu jijini Dar es salaam nchini Tanzania, baada ya chanjo hizo kuwasili nchini humo siku ya Jumamosi kwa msaada wa Marekani kupitia mfumo wa Umoja wa Mataifa wa kusaka chanjo, COVAX

Akizungumza kabla ya kupatiwa chanjo Rais Samia amesema chanjo hizo zimethibitishwa na Wizara ya Afya nchini Tanzania na kwamba chanjo ni imani kwa kuwa “tangu nikiwa shuleni miaka ya 60 tulikuwa tunapatiwa chanjo. Chanjo ya ndui, polio, pepopunda, surua. Na mwilini mwangu nina chanjo kama tano na hii ya leo itakuwa ya sita. Chanjo ni imani, kwa wale wenye mawazo potofu, wizara ya afya na vyombo vya habari na wasanii wetu mfanye kazi ya kuelimisha watu umuhimu wa chanjo. Kwa wale wawanaotaka kuchoma chanjo kwa hiari tutahakikisha kwamba nchi yetu inapata idadi ya kutosha ya chanjo.” 

Waziri wa Afya na wa mambo ya nje wa Tanzania, Balozi wa Marekni na Afisa wa UNICEF wakiwa katika [ocha ya pamoja baada ya makabidhiano ya chanjo ya Corona
UNIC Dar es salaam
Waziri wa Afya na wa mambo ya nje wa Tanzania, Balozi wa Marekni na Afisa wa UNICEF wakiwa katika [ocha ya pamoja baada ya makabidhiano ya chanjo ya Corona

Dozi zilizowasili ni zaidi ya milioni 1 na hivyo Rais Samia akasema wameagiza chanjo zaidi.

Pamoja na chanjo amekumbushia watanzania kuchukua tahadhari ya kujikinga huku akisema, “kwa wale ambao koo zao hazijaguswa, hawajapata athari za maradhi haya,wanaweza kusema watakavyo. Lakini nenda leo  Moshi, Arusha, Kagera na hata hapa Dar es salaam  uonane na zile koo ambazo zimeshaguswa na haya maradhi, wana maneno ya kukuambia, na kama wangaliweza wote wangalikuwepo hapa wapate chanjo. SAsa ndugu zangu kama hujapatwa na  hili janga unaweza kusema lolote, lakini likikugusa unajua hatari ya hili janga.”

Chanjo zilizowasilishwa Tanzania kupitia mpango wa COVAX ni aina ya Johnson & Johnson.

Tanzania ina wagonjwa 682 wa COVID-19

Kwa mujibu wa Waziri wa Afya nchini Tanzania, Dkt. Dorothy Gwajima hadi tarehe 21 mwezi huu wa Julai Tanzania ilikuwa na jumla ya wagonjwa 682.
 

Tarehe 22 mwezi Julai pekee kulikuwa na wagonjwa wapya 176 ambapo ikilinganishwa na wiki mbili zilizopita kulikuwa na wagonjwa 408 hivyo kasi ya maambukizi ni kubwa.
 

Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini Tanzania Salini Bahuguna akizungumza siku chanjo zilipowasili alisema, “napongeza serikali kwa juhudi za kuhakikisha chanjo zinawasili nchini. Hii ni hatua kubwa sana katika kupambana na janga. Chanjo hizi zimefanyiwa utafiti na wataalamu duniani kote, watanzania zipokeeni kwa kuwa hakuna aliye salama hadi kila mtu yuko salama.”
 

Kwa upande wake Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO Dkt. Tigest Mengestu naye amepongeza serikali ya Tanzania kwa kushirikiana kwa karibu na wadau ili kupata chanjo hizo. “Takwimu zinaonesha kuwa chanjo zinaongeza kinga yamwili dhidi ya janga na kwamba kuwa na chanjo hiyo nchini Tanania kutaimarisha afya ya umma.”
 

Kwa mujibu wa WHO, hakuna dalili ya COVID-19 kukaribia kutoweka duniani na sasa dunia iko katika hali tete kwa sababu kuna wagonjwa milioni 191 waliothibitishwa na kati ya hao milioni 4.8 wamefariki dunia. “Takwimu hizi ni za watu halisi kwa hiyo tunahitaji kushirikiana paoja kukabiliana na adui huyu,” amesema Dkt. Mengestu.