Mkataba wa wakimbizi watimiza miaka 70 leo 

28 Julai 2021

Ikiwa leo ni miaka 70 tangu kusainiwa kwa mkataba wa kimataifa wa wakimbizi mwaka 1951, wanufaika wa nyaraka hiyo wanashukuru kwa kuwa bila nyaraka hiyo maisha yao yangalikuwa ya tabu .

Vita, ghasia na mateso vinaendelea kufurusha makwao mamilioni ya watu duniani kote! 

Ndivyo inavyoanza video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, video mahsusi kabisa kwa siku ya leo ya kuadhimisha miaka 70 ya mkataba wa kimataifa kuhusu wakimbizi uliopitishwa tarehe 28 mwezi Julai mwaka 1951. 

Msimulizi ni Maya Ghazal, balozi mwema wa UNHCR ambaye pia ni mnufaika wa mkataba huo kwa kuwa yeye mwenyewe na familia yake walifurushwa na machafuko nchini Syria. 

Maya anasema, “kama mkimbizi kutoka Syria, nafahamu machungu ya kufurushwa nyumbani kwako, na machungu ya safari ya kusaka eneo salama. Mkataba wa kimataifa wa wakimbizi uliwezesha mimi na familia yangu kuweza kupata makazi mapya na kujenga upya maisha yetu.” 

Tangu mwaka 1951, mkataba huo umekuwa msingi wa haki za wakimbizi na umeokoa watu wengi waliolazimika kukimbia makwao. 

UNHCR imekuwa ndio mlinzi au mhifadhi wa mkataba huu tangu mwanzo hadi sasa na inaendelea kuhakikisha kuna hifadhi ya kimataifa kwa watu waliofurushwa kutoka nyumbani kwao. 

Maya anasema, “baada ya miaka 70, mkataba huu bado una umuhimu kuliko wakati wowote ule. Unatoa mwongozo kwa nchi juu ya ulinzi wa wakimbizi, na unatoa wito wa ushirikiano wa kimataifa na kusaidia hatua za kusaidia wakimbzi.” 

 Hadi sasa mkataba huo umetiwa saini na nchi 149 na matarajio ni kwamba nchi zaidi zitatia saini na kuridhia. 

Maya anaendelea akisema, “kwa kuzingatia idadi kubwa ya watu wanaovuka mipaka, mito, majangwa na baharí ili kusaka usalama, ni muhimu sana nchi zote zikatia saini mkataba huo.” 

 Anatamatisha kwa kusema  “bila mkataba  huo, nisingalikuwa na uhuru na utulivu ninaofurahia hivi sasa. Mimi na mamilioni ya wengine tusingalikuwa na fursa ya kujijenga upya na kupata elimu au amani na matumaini. Mkataba huu unaweza kuonekana ni maandishi tu lakini kwa wakimbizi umebeba mambo mazuri. Unaruhusu sote kuota ndoto ambayo siku moja wale waliolazimika kukibia wanaweza kupata pahali wanaita nyumbani.” 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter