Uwekezaji wa kupambana na ugonjwa wa homa ya ini wazaa matunda

28 Julai 2021

Leo ni siku ya Homa ya ini duniani, Shirika la kimataifa la kufanikisha upatikanaji wa tiba nafuu, UNITAID ambalo ni shirika tanzu la shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO inaadhimisha maendeleo yaliyofanywa katika kufikia malengo ya kutokomeza ugonjwa huo.

Homa ya Ini ni ugonjwa unaoambukizwa na virusi kwenye damu ambavyo vinaweza kusababisha uharibifu mkubwa wa ini, na ukiachwa bila kupatiwa tiba mgonjwa anaweza kupata ugonjwa wa saratani.

Video ya Shirika la UNITAID inamuonesha mgonjwa akichukuliwa vipimo mdomoni. Duniani kote  inakadiriwa watu milioni 58 wameambukizwa virusi vya homa ya ini lakini ni asilimia 21 pekee ndio wamefanyiwa  uchunguzi.

Mkurugenzi wa mikakati wa UNITAID Janet Ginnard anasema sasa upimaji ni rahisi

“UNITAID imethibitisha kuwa upimaji rahisi na matibabu ya homa ya ini katika vituo vya kutolea huduma za afya sio tu unawezekana lakini hata katika sehemu zisizo na uwekezaji mkubwa bado kunaweza kuwa na ufanisi mkubwa. Zaidi ya dola milioni 45 zimewekezwa tangu mwaka 2015, tumenunua dawa za bei ya chini, tumerahisisha upimaji huku tukiongeza ufahamu wa ubunifu. Njia hizi, ikiwa zitatekelezwa kwa kiwango kikubwa, zitaweza kuepusha maelfu ya vifo vinavyohusiana na homa ya ini kila mwaka ”

Habari njema ni kuwa tayari wameona matokeo chanya ya uwekezaji huo,

“Tayari tunaona maendeleo yanayotia moyo ambayo yanatuonesha kwamba kufikia malengo ya shirika la Afya ulimwenguni WHO inawezekana. Tangu mwaka 2015, vifo vinavyohusiana na  homa ya ini vimepungua kwa zaidi ya asilimia 25, na idadi ya watu walioambukizwa imeshuka kutoka milioni 71 hadi milioni 58 leo. Shukrani ziende si kwa UNITAID pekee bali na washirika wetu, sasa tuna vifaa tunavyohitaji kupambana na homa ya ini na kufikia malengo haya, lakini, hakuna wakati wa kupoteza.”

Inakadiriwa watu 290,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na ugonjwa huu. Watu walio kwenye mazingira duni, masikini, wanaotumia dawa za kulevya na wale wanaoishi na virusi vya UKIMWI wapo katika hatari kubwa ya kuambukizwa homa ya ini

WHO imeweka malengo ifikapo mwaka 2030 ugonjwa wa homa ya ini uwe umeondolewa kwenye magonjwa ambayo ni tishio la afya ulimwenguni.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter