Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 imebadili taswira ya elimu kwa watoto : UNICEF

Watoto wakimbizi wa ndani huko Cabo Delgado, Msumbiji
© UNICEF/Daniel Timme
Watoto wakimbizi wa ndani huko Cabo Delgado, Msumbiji

COVID-19 imebadili taswira ya elimu kwa watoto : UNICEF

Utamaduni na Elimu

Janga la Corona limesababisha zaidi ya watoto milioni 600 katika nchi ambazo hawako kwenye mapumziko, kuendelea kuathiriwa na kufungwa kwa shule.

Katika hali ya kawaida shuleni watoto wanapata elimu, wanakuwa salama, wanapata marafiki na kwingineko chakula, lakini janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 limebadili hayo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto hii leo linasema hivi sasa hali imekuwa ni wasiwasi, Vurugu na mimba katika umri mdogo. 

Akizungumza na vyombo vya habari akiwa mjini Geneva, Uswisi msemaji wa UNICEF  James Elder amesema “janga la Corona limesababisha zaidi ya watoto milioni 600 katika nchi ambazo hawako kwenye mapumziko, kuendelea kuathiriwa na kufungwa kwa shule.” 

Akitolea mfano wa namna watoto walivyoathiriwa na kufungwa kwa shule Elder amesema “katika nchi kama Uganda, ufungaji shule umesababisha kuongezeka kwa mimba katika umri mdogo kwa asilimia 20 ndani ya kipindi cha miezi 15, mabinti ambao walikuwa wakitafuta huduma ya ujauzito ni umri kati ya miaka 10-24. Na ulimwenguni kote katika mabara yote, tumeona namba zilizowekwa kwa ajili ya kutoa msaada kwa watoto, watoto kuripoti vurugu, kumekuwa na ongezeka la tarakimu tatu” 


 Kufungwa kwa shule sababu ya janga la COVID-19 

Mpaka kufikia hii leo, UNICEF inakadiria mashariki na kusini mwa bara la Afrika asilimia 40 ya watoto wote wenye umri wa miaka 5 hadi 18 hawaendi shule.

Karibu nusu ya nchi za Asia na Pasifiki, shule zimefungwa kwa takriban siku 200. Upande wa Amerika ya kusini na visiwa vya Karibea shule zimefungwa kwa muda mrefu zaidi zikiwemo nchi 18 , na nyingine zilizofungwa ama kabisa au kufungwa nusu na nusu wanafunzi wakiendelea na masomo.

Elder amesema” kama takwimu hizi hazitawashtua walioko madarakani , basi ripoti ya Benki ya Dunia inakadiria hasara ya dola trilioni 10 ya mapato kwa kizazi hiki cha wanafunzi.” 

Angures Buba (kulia) na mwenzake wakisikiliza matangazo ya shule kwa njia ya redio huko Sudan Kusini.
© UNICEF/Helene Sandbu Ryeng
Angures Buba (kulia) na mwenzake wakisikiliza matangazo ya shule kwa njia ya redio huko Sudan Kusini.

 Kuendelea na masomo wakiwa nje ya shule hakuwafikii wengi 

Msemaji huyo wa UNICEF amesema suala la watoto kusomea majumbani limekuwa haliwezekani kwa sehemu kubwa ambapo takwimu zinaonesha theluthi moja ya watoto duniani hawapati fursa hiyo.

“Mashariki na kusini mwa Afrika, watoto wa shule za nchini Uganda wamekaa siku zaidi ya 300 bila ya kwenda shule. Upatikanaji wa huduma za mtandao wa intaneti majumbani upo chini zaidi ulimwenguni kwani upo kwa asilimia 0.3.” 

“Katika ukanda wa Asia mashariki na Pasifiki ,watoto milioni 80 hawana fursa yoyote ya kuwawezesha kusoma wakiwa mbali na shule.” 
Hali hii haiwezi kuendelea 

Zaidi ya watoto milioni 100 watakuwa chini vya viwango vya kujua kusoma kutokana na athari za janga la Corona lililosababisha shule kufungwa
© UNESCO/Dana Schmidt
Zaidi ya watoto milioni 100 watakuwa chini vya viwango vya kujua kusoma kutokana na athari za janga la Corona lililosababisha shule kufungwa


 Katika kutoa ushauri nini kifanyike, UNICEF imetaja hatua kuu tano.

1.    Shule zifunguliwe haraka iwezekanavyo 
2.    Serikali na wafadhili lazima walinde bajeti ya elimu 
3.    Uandikishaji wa wanafunzi unapaswa kuzingatia pia watoto ambao walikuwa nje ya shule kabla ya janga la COVID-19 kwa kuondoa vizuizi 
4.    Kulegeza masharti ya usajili 
5.    Uhamisho kwa wanafunzi walio katika hatari unapaswa kuongezwa. 

“kila kitu kinahitajika kufnayika ili kumaliza hili janga” amesema Elder akihimiza na kuanza kwa kuhakikisha chanjo inapatikana kila mahali kwa kushiriki kuchangia dozi nyingi ili kuhakikisha upatikanaji wa chanjo kote duniani.