Skip to main content

Tunashindwa kutimiza haki ya msingi ya watu: Amina Mohammed

Amina Mohammed, Naibu katibu mkuu  wa Umoja wa Mataifa, akihutubia katika mkutano wa awali wa mifumo ya chakula 2021 Roma, Italia
UN Photo/Giulio Napolitano
Amina Mohammed, Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, akihutubia katika mkutano wa awali wa mifumo ya chakula 2021 Roma, Italia

Tunashindwa kutimiza haki ya msingi ya watu: Amina Mohammed

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed amefungua mkutano wa utangulizi wa mifumo ya chakula mjini Roma, Italia, na kuzishawishi nchi zote duniani kuhakikisha zinaweka mifumo mizuri ya chakula ili kuhakikisha malengo ya maendeleo endelevu SDGs yanafikiwa mwaka 2030 kwavkuwa janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 limerudisha nyuma mipango mingi. 

Akitaja takwimu mbalimbali amesema ripoti ya mwaka 2020 inaonesha mabadiliko ya tabianchi yamesababisha takriban watu bilioni 2.37 duniani kote kukosa chakula cha kutosha ikiwa ni ongezeko la watu milioni 320 ikilinganishwa na mwaka 2019. 

“Jambo hili hakuna mtu hata mmoja alitegemea, ukizingatia tuna mbinu za kupambana na matatizo ya ulimwengu. Watu bilioni 3 wameshindwa kumudu kupata lishe bora, haya yote yanatokea wakati changamoto za hali ya hewa zinazidi kuongezeka. Tunashindwa kutimiza haki ya msingi ya watu, pia tunaifanya sayari yetu ishindwe” amesema Amina Mohammed wakati akitoa rai kwa viongozi mbalimbali walio hudhuria mkutano huo. 

“Tunaona pia uongozi wa kikanda. Kila kanda wanatafuta mbinu za kipekee zinazoendana na mahali ya eneo lao katika kuainisha vipaumbele vya kushirikiana na kuchukua hatua. Nchi wanachana, ikiwemo kamati za usalama wa chakula ulimwenguni, na zile zenye makazi yake hapa mjini Roma zinasaidia katika majadiliano hayo ili kuhakikisha kila mmoja anajufaika na mbinu zinazokubaliwa na zinazoweza kutekelezeka.”

Naibu katibu mkuu huyu pia ameeleza wadau na wataalamu wamechangia na kuwasilisha mawazo na mbinu zaidi ya 2000 ambazo zitasaidia katika kushughulikia mifumo ya chakula.

“Nimefarijika na nguvu mliyoweka kwenye suala hili. Lakini kuna mengi yanahitajika kufanyika katika siku 3 zijazo za mkutano ili tutoke na makubaliano yenye matokeo ambayo yatatoa muelekeo kwenye mkutano wa viongozi mwezi Septemba mjini New York, Marekani.” 

Amehitimisha hotuba yake kwa kusisitiza kuwa chakula lina unganisha kila mmoja, familia, jamii, tamaduni na ubinadamu. Na kuhimiza huu ni muda wa kuungana katika dharura hii na kuchukua hatua zote zinazohitajika kuibadili dunia ifikapo mwaka 2030.