Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Homa ya ini, Hepatitis yaua mtu 1 kila sekunde 30

Mama na mwanawe katika kituo cha afya cha mama na mtoto huko Mauritania wakati wa Wiki ya Chanjo ya Ini ya aina ya B.
© UNICEF/Raphael Pouget
Mama na mwanawe katika kituo cha afya cha mama na mtoto huko Mauritania wakati wa Wiki ya Chanjo ya Ini ya aina ya B.

Homa ya ini, Hepatitis yaua mtu 1 kila sekunde 30

Afya

Katika kila sekunde 30 mtu mmoja anafariki dunia kutokana na ugonjwa wa homa ya ini, au Hepatitis, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO katika taarifa zake kuelekea siku ya kimataifa ya ugonjwa huo hatari lakini ambao bado umma haujawa na taarifa za kutosha kuhusu hatari zake.
 

 

Soundcloud

Ujumbe wa mwaka huu wa siku hiyo ya homa ya ini duniani inayoadhimishwa kila tarehe 28 ya mwezi Julai ni “homa ya ini haiwezi kusubiri” ikiwa ni katika kuchagiza kuhusu umuhimu wa juhudi za haraka kwa ajili ya kutokomeza homa ya ini kuwa tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030.

WHO inasema licha ya uwepo wa ugonjwa wa Corona au COVID-19,  lazima kuwepo na juhudi za makusudi za kukabiliana na magonjwa mengine ikiwemo homa ya ini ambao ni  ugonjwa unaombukiza. 
Muuguzi kutoka hospitali kuu ya Taifa, Kenyatta nchini Kenya Daniel Otieno akizungumza na Grace Kaneiya wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, jijini Nairobi ametaja aina za homa ya ini kuwa ni A, B, C, D na E.
Hata hivyo amesema aina zinazotambulika zaidi na hatari zaidi ni B na C yaani Hepatitis B na Hepatis C, “kwa sababu iwapo mgonjwa hatopatiwa tiba ya haraka dhidi ya aina hizi mbili anaweza kupoteza maisha. Hizi mbili njia zake za maambukizi zinafanana na zinaweza kuenea hata kwa mtoto ambaye yuko tumboni mwa mama yake ndio maana tunapatia  umuhimu zaidi.”

Matumizi ya tena na tena ya sindano huhatarisha maambukizi ya homa ya ini.
IRIN/Kamila Hyat
Matumizi ya tena na tena ya sindano huhatarisha maambukizi ya homa ya ini.

Akizungumzia njia za maambukizi, Bwana Otieno amesema, “kwa upande wa homa ya ini aina ya B, maambukizi yake ni mara 100 kulinganisha na virusi vya Ukimwi. Ni ugonjwa ambao unaweza dhuru binadamu lakini watu bado hawajaweka mkazo sana. Ni kwa sababu haijapatiwa taarifa ya kutosha, lakini inaua watu wengi na njia ambazo unaweza kuambukizwa ni pamoja na kudungwa sindano iliyokwishatumika na mtu aliyekuwa na virusi vya Hepatitis B.  Pia kwa njia ya ngono iwapo mmoja ana virusi vya Homa ya ini. Mama mjamzito pia akiwa na virusi vya homa ya ini anaweza kumuambukiza mtoto tumboni au wakati anazaliwa.”

Bwana Otieno amesema njia za maambukizi ya homa ya ini  zinafanana na zile za Virusi Vya Ukimwi au VVU. “Lakini kinachotufanya tuwe makini zaidi ni kwamba ni rahisi mara 100 zaidi kuambukizwa virusi vya Homa ya Ini kuliko VVU.”

Hata hivyo amesema kuna njia za kinga na tiba. Ikiwemo chanjo dhidi ya homa ya ini na wagonjwa wanapona. Kuzuia ni pamoja na kuhakikisha hakuna kutumia sindano baada ya kutumika mara moja. Pia mtu asiwe na tabia ya kufanya ngono kiholela “kwa sababu unaweza kukutana na mtu mwenye virusi na akuambukize. Halikadhalika mtu apime kwa maabara ajue kama ana virusi vya homa ya ini au la.”