Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna njia ya kufikia Mkataba wa Paris wa lengo la nyuzi joto 1.5˚C bila G20 – Katibu Mkuu UN 

Mafuriko yanaongezeka ulimwenguni kote kutokana na mabadiliko ya tabianchi
UN Women/Mohammad Rakibul Hasan
Mafuriko yanaongezeka ulimwenguni kote kutokana na mabadiliko ya tabianchi

Hakuna njia ya kufikia Mkataba wa Paris wa lengo la nyuzi joto 1.5˚C bila G20 – Katibu Mkuu UN 

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo Jumapili amesema, "Ulimwengu unahitaji haraka kujitolea kwa mataifa yote ya G20 kuliko wazi na kusiko na utata kwenye lengo la nyuzi joto 1.5 za selisiasi la Mkataba wa Paris.”  

Bwana Guterres ameyasema hayo baada kundi la nchi ishirini tajiri, G20 kushindwa kukubaliana kuhusu ahadi muhimu za mabadiliko ya tabianchi wakati wa Mkutano wao wa Mawaziri uliofanyika tarehe 23-25 mwezi huu wa Julai kuhusu Mazingira, Mabadiliko ya tabianchi na Nishati.  

“Hakuna njia ya kufikia lengo hili bila uongozi wa G20. Ishara hii inahitajika sana na mabilioni ya watu ambao tayari wako kwenye mstari wa mbele wa tatizo la mabadiliko ya tabianchi na kwa masoko, wawekezaji ambao wanahitaji uhakika kwamba hali halisi ya mabadiliko ya tabianchi inayoweza kuepukika haikwepeki .” Amehimiza Bwana Guterres. 

Mawaziri wa G20, ambao walikutana huko Naples, Italia tarehe 23-25 ya mwezi huu wa Julai, hawakuweza kuafikiana kuhusu masuala mawili juu yenye utata yanayohusiana na kumaliza makaa ya mawe na lengo la nyuzi joto 1.5, ambayo sasa italazimika kujadiliwa katika mkutano wa G20 huko Roma mnamo Oktoba, siku moja tu kabla ya COP 26 kuanza. 

Aidha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekumbushia kwamba sayansi inaonesha kwamba kufikia 'azma hiyo kubwa, lakini ambayo inaweza kufikiwa’, ulimwengu lazima ufikie kutokuwepo kwa hewa chafuzi kabla ya mwaka 2050 na kupunguza uzalishaji hatari wa hewa chafuzi kwa asilimia 45 ifikapo mwaka 2030 kutoka viwango vya mwaka 2010. "Lakini bado tuko mbali sana." Ameonya. 

Zikiwa zimesalia chini ya siku 100 kabla ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi wa 2021, COP 26, mkutano muhimu ambao utafanyika Glasgow mwishoni mwa Oktoba, António Guterres amewahimiza G20 wote na viongozi wengine kujitolea kufikia lengo.