Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakulima Ethiopia waeleza namna wanavyotaka changamoto za kilimo zitatuliwe 

Mifumo ya chakula barani Afrika imevurugwa kwa kiasi kikubwa kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi na hivi karibuni zaidi janga la Corona.
© FAO/Petterik Wiggers
Mifumo ya chakula barani Afrika imevurugwa kwa kiasi kikubwa kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi na hivi karibuni zaidi janga la Corona.

Wakulima Ethiopia waeleza namna wanavyotaka changamoto za kilimo zitatuliwe 

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchini Ethiopia, Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya Kilimo IFAD unatekeleza kwa vitendo lengo namba 13 la malengo ya maendeleo endelevu SDGs, la hatua kwa tabianchi, kwa kuwafuata wakulima mashambani na kusikiliza changamoto walizokutana nazo na namna wanavyotaka zitatuliwe. 

Nchini Ethiopia, video ya Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya Kilimo IFAD inamuonesha Temesgen Tchane mkulima wa zao la ngano akiwa shambani ambako anaeleza changamoto wanazokutana nazo wakulima wa mazao ya lishe. “Tuna uoga na wasiwasi mkubwa kuwa kipato chetu mwisho wa mwaka kitapungua. Ukifika msimu wa upanzi, tunakuwa hatuna muda wa kutosha kuondoa magugu vamizi au “boukaya”. Tungetamani sana kupata vifaa au mashine ambazo zingetusaidia kuyaondoa.  Lakini pia kwa miezi inayokuja, kadiri tunavyokaribia msimu wa mvua, tunaanza kuingiwa na wasiwasi kuwa mvua zitaharibu mazao yetu.” 

Sasa nini kifanyike ili kusaidia maisha ya wakulima yawe rahisi zaidi? “Kama tutapata fursa ya kupata mashine na kutengeneza vikundi vidogo ambavyo mtatusaidia na kutuwezesha kununua mashine hii itatusaidia.” 

Mabadiliko ya tabia nchi nayo yamemuathiri akisema,“Mabadiliko ya tabia nchi yameleta ukame, na kupunguza uwezo wetu wa kupata maji. Na hii imeathiri pia zao letu la ngano. Tungependa kupata mbegu za zao la ngano za muda mfupi, na pia kupata msaada wa kuunganishwa na wazalishaji wa mbegu hizo ili tuweze kuzinunua. “ 

Kando mwa changamoto hizo, Tchane ana matumaini na maisha ya baadaye “Nataka kuelimisha watoto wangu, ili niipe fursa familia yangu kukua zaidi na kuwa na maisha ya baadaye bora zaidi ili hatimaye waweze kuleta mabadiliko.”