Hali ya chanjo ilikuwa mbaya wilaya ya Mzimba, Malawi kabla ya UNICEF kuingilia kati

22 Julai 2021

Baada ya  utafiti kuonesha kushuka kwa kiasi kikubwa cha watoto kupata chanjo katika wilaya ya Mzimba nchini Malawi,  hatua iliyochukuliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kuanzia mwaka 2017, sasa inaonesha kuzaa matunda kwani idadi ya watoto wanaochanjwa na uelewa wa wazazi kuhusu chanjo vimepanda.

Katika eneo la Kusini la Wilaya ya Mzimba, ni moja ya maeneo yenye ugumu wa kufikika nchini Malawi. Wanawake wanaonekana wakitembea wakikatisha katika vinjia vidogo katika vichaka na mashamba na hatimaye kutokea katika kituo cha chanjo. Kivuli cha miti kinawapumzisha, wakisubiri watoto wao wachanjwe. 

Steve Macheso ni mtaalam wa afya wa UNICEF nchini Malawi anasema moja ya hatua muhimu za kiafya za kuhakikisha maisha ya watoto ni chanjo kwa hivyo kiasi cha wanaochanjwa kikishuka kufikia asilimia 69 kama walivyogundua mwaka 2017, inafungua milango ya magonjwa kujitokeza na ndio maana UNICEF kwa kushirikiana na Wizara ya afya ya Malawi iliamua kusaidia mradi huu kiufundi na kiuchumi.  

Antonios Madhlopa ni mshauri wa afya katika eneo la Mzimba Kusini akizungumzia namna UNICEF ilivyoleta nuru katika eneo hilo anasema, “unapozungumzia chanjo ni kwa sababu ya UNICEF. Ukizungumzia majokofu ni UNICEF. Ukizungumzia maarifa na ujuzi wa wafanyakazi wa afya, ni kwa sababu ya UNICEF.” 

Modesta Banda ni mmoja wa akina mama wa Mzimba Kusini anasema,  "Tunapoenda kliniki, tunaambiwa kuwa watoto ambao wamepewa chanjo wana maisha mazuri ya baadaye kwa sababu wanalindwa dhidi ya maambukizi na magonjwa, tofauti na wale ambao hawajachanjwa, maisha yao ya baadaye hayana hakika kwa sababu wanakosa ulinzi katika miili yao." 

Steve Macheso Mtaalam wa Afya wa UNICEF nchini Malawi akithibitisha namna hatua zilizochukuliwa zilivyozaa matunda anasema,  "Kwa kutazama taarifa za hadi mwaka jana 2020, uchanjaji watoto katika eneo hili umepanda hadi asilimia 82, na hapo ndio nataka iwe." 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter