Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yawajengea nyumba wakimbizi wa ndani DRC

Familia zilizofurushwa kwa ajili ya mzozo mashariki mwa DRC wanapatiwa msaada wa kibinadamu na mashirika ya UN.
© UNICEF/Jean-Claude Wenga
Familia zilizofurushwa kwa ajili ya mzozo mashariki mwa DRC wanapatiwa msaada wa kibinadamu na mashirika ya UN.

UNHCR yawajengea nyumba wakimbizi wa ndani DRC

Wahamiaji na Wakimbizi

Machafuko yanaendelea Jimbo la Kivu kaskazini nchini Jamhuri ya kidemokrasia Kongo, DRC yanasababisha kila uchwao wananchi wa eneo hilo kuyakimbia makazi yao kwenda kuishi mikoa ya jirani.

Pamoja na kukaribishwa huko wanapokimbilia changamoto kubwa inakuwa mahali pakuishi.  Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limeamua kuwajengea wananchi hao makazi ya muda mrefu. Tuungane na Leah Mushi kupata taarifa zaidi.

Shughuli ya ujenzi wa nyumba kwa ajili ya wakimbizi wa ndani chini ya ufadhili wa UNHCR inaendelea. Elodie anakumbuka safari ya tabu akiwa na Watoto wake.

“Watoto wangu na mimi tulitembea kwa siku mbili kwa miguu. Hatukuwa na chakula na hatukuwa na pesa ya kulipa kupanda taxi. Watoto wangu miguu ilivimba na miguu ilikuwa inatuuma sababu ya safari kuwa ndefu sana”

Walipofika eneo hili waliishi kwenye hema lilikuwa linavuja kwa muda wa miezi nane, UNHCR Pamoja na wadau wake sasa wanawapatia huduma ya chakula, matibabu na makazi ya kudumu.

“Hizi nyumba zimetusaidia sana na tupo salama. Pale tulipokuwa tunaishi awali, tulikuwa tunanyeshewa na mvua muda wote na hatukuwa na mahali pa kulala. Sasa tumetulia.”

Afisa wa UNHCR anayesimamia eneo hili la Beni, Ibrahima Diane, anasema wanahakikisha kuna umoja“Tunasaidia katika dharura, tunawasaidia mahitaji wakimbizi wa ndani waliofika hapa ili waweze kujijengea makazi ya dharura, lakini pia tuliboresha hali ya eneo hili kwa kutoa msaada kwa jamii ili waweze kupata makazi sawa na yaliyopo katika jamii. Jambo hili limewezesha kuwa na umoja baina yao na jamii iliyowakaribisha katika eneo hili.”

Mwaka jana 2020 UNHCR ilijenga makazi zaidi ya laki 1, na tangu Januari mwaka huu (2021) imeshajenga zaidi ya makazi elf 14 kwa ajili ya wakimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo, DRC.