Henrietta Fore atangaza kujiuzulu UNICEF, Guterres akubali

15 Julai 2021

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF Henrietta Fore, amemjulisha Katibu Mkuu wa umoja huo, Antonio Guterres juu ya nia yake ya kujiuzulu wadhifa wake kutokana na suala la afya la kifamilia.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa jijini New York, Marekani na Farhan Haq ambaye ni Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu imesema Guterres amekubali uamuzi huo akisema anaelewa fika lakini amekubali kwa masikitiko makubwa.

Amemshukuru Bi. Fore kwa utendaji wake huku akitakia kila la kheri familia yake.

“Katibu Mkuu anapenda kuelezea shukrani zake za dhati kwa Bi. Fore kwa uongozi wake UNICEF wa kutia hamasa sambamba na huduma yake ya kuboresha maisha ya watoto duniani,” imesema taarifa hiyo.

Mkuu wa UNICEF Henrietta H. Fore akiwa katika wadi ya watoto mjini Sana'a Yemen
© UNICEF/UN0219817/
Mkuu wa UNICEF Henrietta H. Fore akiwa katika wadi ya watoto mjini Sana'a Yemen

Bwana Guterres ametolea mfano nafasi muhimu ya UNICEF katika hatua zake za kimataifa za kupambana na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 sambamba na kufikiria upya suala la elimu.
 
“Ni kutokana na uongozi wake, UNICEF hivi sasa ni shirika lenye taswira pana katika ubia na sekta ya umma na binafsi na mtazamo jasiri wa kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs,” amesema Guterres.

Ameenda mbali akisema Bi. Fore amechangia kwa kiasi kikubwa juhudi za kujenga upya mfumo wa Umoja wa Mataifa ukiwa na mtazamo thabiti wa ujumuishi na utamaduni wa kishirika.

Guterres amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNICEF kwa utumishi uliotukuka katika kushughulikia changamoto zinazokumba watoto na vijana barubaru duniani kote.
 
Bi. Fore alianza jukumu lake la  Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF tarehe 1 mwezi Januari mwaka 2018 na ataendelea kushikilia wadhifa huo hadi atakayeshika wadhifa huo atakapoteuliwa.

TAGS: UNICEF, Henrietta Fore
 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter