Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Stadi za vijana ziimarishwe ili kukwamuka vizuri baada ya COVID-19

 Bernad Kagwe, kijana kutoka Kenya ambaye yeye na wenzake wamebuni kifaa hicho cha kuwezesha mtu kupata kitasaka mikono bila kushika popote kwa lengo la kudhibiti kuenea kwa virusi vya Corona.
UN/ Jason Nyakundi
Bernad Kagwe, kijana kutoka Kenya ambaye yeye na wenzake wamebuni kifaa hicho cha kuwezesha mtu kupata kitasaka mikono bila kushika popote kwa lengo la kudhibiti kuenea kwa virusi vya Corona.

Stadi za vijana ziimarishwe ili kukwamuka vizuri baada ya COVID-19

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Leo tunasherehekea mnepo wa vijana, hamasa na ubunifu wao wakati wa janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19. Ndivyo alivyoanza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku ya leo ya kimataifa kuhusu stadi kwa vijana ikiwa na ujumbe kufikiria upya stadi za vijana baada ya janga la Corona.

Guterres amesema “vijana hata kabla ya janga la Corona, tayari walikuwa wanakabiliwa na kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira. Zaidi ya kijana 1 kati ya 5 alikuwa hana ajira, elimu au mafunzo na wengi wao walikuwa vijana wa kike.”

Katibu Mkuu amesema janga la Corona ni kama lilitia chumvi kwenye kidonda kwa kuwa lilizidi kuwaweka vijana katika hali ngumu. “Katika matukio mengi, janga la Corona lililazimu mashirika kusitisha mafunzo ya stadi. Mafunzo kwa njia ya mtandao nayo yalikuwa ni kikwazo kwa vyuo vya mafunzo stadi hususan kwa vijana walio pembezoni.”

Ni kwa mantiki hiyo, Katibu Mkuu anataka iwapo dunia inataka kuibuka vyema na kwa uendelevu kutoka janga la Corona ni lazima kupatia suluhu ukosefu wa usawa uliodumu muda mrefu na changamoto ambazo vijana wanakabiliana nazo.

“Hii inamaanisha kuchagiza uendelezaji wa stadi na elimu, hususan hatua dhidi ya madhara ya tabianchi, usawa wa jinsia na ujumuishi. Ni muhimu sana kuongeza uwekezaji katika mafunzo ya ufundi stadi, teknolojia ya mawasiliano na stadi za kidijitali,” amesema Katibu Mkuu.

Amekumbusha vijana wana suluhu na hivyo ni lazima wawe kwenye meza za maamuzi ikiwemo michakato ya utungaji wa sera katika ngazi ya kijamii, kitaifa na kimataifa. “Mkakati wa Umoja wa Mataifa kwa vijana wa mwaka 2030 au #Youth2030 umeweka mwelekeo kwa Umoja wa Mataifa na wadau wake kushirikiana kwa pamoja il ikujenga maendeleo endelevu yaliyo sawa na kwa wote.”

Ametamatisha ujumbe wake Katibu Mkuu kwa kuitakia jamii ya kimataifa siku njema ya stadi kwa vijana.