Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yasababisha watoto milioni 23 kukosa chanjo

Msichana akipokea chanjo wakati wa kampeni ya chanjo nchini Venezuela.
PAHO
Msichana akipokea chanjo wakati wa kampeni ya chanjo nchini Venezuela.

COVID-19 yasababisha watoto milioni 23 kukosa chanjo

Afya

Watoto milioni 23 duniani mwaka jana wa 2020 walikosa huduma muhimu ya chanjo zinazotolewa kuwakinga dhidi ya maradhi mbalimbali, idadi hiyo ikiwa ni ongezeko la watoto milioni 3.7 ikilinganishwa na mwaka 2019, yamesema mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa lile la kuhudumia watoto UNICEF na lile la afya, WHO.

Huduma za chanjo zikiendelea hapa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, taarifa iliyotolewa kwa pamoja  hii leo na UNICEF nchini Marekani na WHO nchini Uswisi  inaonesha kuwa watoto hao zaidi ya milioni 23 ulimwenguni kote walikosa chanjo muhimu za magonjwa kama surua, pepopunda na polio kwa mwaka jana 2020. 

Akiwa katika kliniki ya mama na mtoto ya Kinkole jijini  Kinshasa nchini DRC, Dkt. Tessi Mvutukulu, Mganga Mkuu wa Idara ya Watoto, amesema idadi ya watoto wanaoletwa kliniki imepungua sana kwa hofu itokanayo na taarifa za uongo kuhusu janga la Corona. “Kuna uzushi umesambaa kupitia mitandao ya kijamii juu ya jaribio la chanjo dhidi ya chanjo ya COVID-19 huko DRC. Watu wanadhani  watatumika kwa majaribio ya chanjo, watu wanawaogopa wahudumu wa afya kwa kusema sisi ni washirika katika kufanya majaribio”. 

Nchi zilizoripotiwa kuongezeka kwa idadi ya watoto ambao hawajapata chanjo ni India, Pakistan, Indonesia, Ufilipino, Mexico, Msumbiji, Angola, Tanzania, Argentina, Venezuela na Mali. 

 

Binti akichomwa chanjo ya polio na surua nchini Iraq baada ya kukimbia machafuko kaskazini mashariki mwa Syria
© UNICEF/Anmar Rfaat
Binti akichomwa chanjo ya polio na surua nchini Iraq baada ya kukimbia machafuko kaskazini mashariki mwa Syria

Taarifa hizo zimetajwa kwenye ripoti ya WHO na UNICEF ikisema   zaidi ya watoto milioni 17 hawajapata hata chanjo moja ya kinga.  

Dkt Ann Lindstrand ni mkuu wa Mipango muhimu na chanjo wa WHO. “Kuvurugika kwa ratiba za utoaji chanjo kumetokea katika nchi nyingi duniani wakati wa janga la Corona. Sababu ni nyingi.Shida ya usafirishaji , hofu ya kutoaminiwa na kuogopa kupata maambukizi ya Corona katika vituo vya afya. Lakini pia watoa huduma wa vituo vya afya walitawanywa, walipelekwa maeneo ya kukabili Corona. Haya yote ukiyaweka pamoja yalihatarisha utoaji huduma wa chanjo kwa kawaida.” 

  Dkt. Lindstrand ameeleza nini kifanyike,"Kinachohitajika sasa ni kwa nchi zote kuangalia huduma zao za chanjo, kurudisha chanjo, kupata watoto wale ambao walipotea wale ambao hawakufikiwa au hawakufikiwa na chanjo katika mwaka huu wa janga. Na wapate chanjo ambazo zinahitajika..” 

Amesema bila chanjo kuna uwezekano wa kupata milipuko mingi ya magonjwa. 

Tafiti pia zimeonesha mbali na wazazi kuogopa kupeleka watoto kliniki kupata chanjo, kwingineko vituo vya afya vilifungwa huku vingine vikipunguza muda wa kufanya kazi.