Walichopoteza watoto baada ya shule kufungwa kutokana na COVID-19 watakipataje? – Ripoti

Kufunguliwa kwa shule na vyuo vya elimu baada ya kufungwa mwaka jana kutokana na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 kumeacha baadhi ya wanafunzi katika njiapanda kwa sababu kile walichopoteza wakati shule zimefungwa , bado hakuna jitihada za kutosha kuhakikisha wanakipata ili kuepusha kukosa kabisa ufahamu wa kile walichokuwa wamepangiwa kukifahamu, imesema ripoti mpya iliyotolewa leo na mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau.
Ripoti hiyo iliyotolewa leo Paris Ufaransa, Washington DC na New York, Marekani inafuatia utafiti wa kuanzia Februari hadi Mei 2021 katika nchi 142 ambako imeonekana kuwa nchi 1 kati ya 3 bado haijaweka mpango wa kuhakikisha wanafunzi wanapata kile walichokosa shule zilipofungwa.
Ni theluthi moja tu ya nchi hizo zimechukua hatua kuhakikisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanajifunza walichokosa na shule hizo ziko katika nchi za kipato cha juu, imesema ripoti hiyo iliyoandaliwa na Benki ya Dunia, mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la elimu, UNESCO na la kuhudumia watoto, UNICEF na shirika la maendeleo ya ushirikiano wa kiuchumi, OECD.
Silvia Montoa, Mkurugenzi wa takwimu UNESCO amesema “kupima kiwango cha mafunzo kilichopotea ni hatua muhimu ya kwanza ya kupunguza athari. Ni muhimu nchi kuwekeza katika kutathmini kiwango cha kile kilichopotea ili kuibuka na mikakati sahihi.”
Katika nchi za kipato cha chini na kati, ni chini ya theluthi moja ya nchi hizo ziliripoti watoto kurejea shuleni na hivyo kuongeza hatari ya kutowekupo zaidi shuleni na utoro.
Hata hivyo baadhi ya nchi hizo zimetumia mbinu za kushawishi wanafunzi kurejea shuleni ikiwemo uhamasishaji kwenye jamii, kuboresha huduma za kujisafi, kupatia shule fedha na ufuatiliaji mahudhurio shuleni.
Kufungwa kwa shule kuliibua matumizi ya kusoma kwa njia ya redio, televisheni na mtandaoni ambapo Robert Jenkins ambaye ni Mkuu wa kitengo cha elimu duniani UNICEF amesema bado hatua hiyo ilikuwa tatizo kwa watoto wengi walio hatarini ambao hawakuweza kuipata.
“Ni suala la dharura kila mtoto arejee darasani sasa. Lakini hatuwezi kuishia hapa. Kufungua shule kwa hatua bora zaidi kunamaanisha kutekeleza mipango ya kurekebisha na kusaidia wanafunzi kurejea vyema na kuhakikisha tunapatia kipaumbele wasichana na watoto walio hatarini,” amesema Jenkins.
Ripoti hii imezinduliwa leo wakati wa mkutano wa mawaziri kuhusu elimu duniani.
Nchi zimechukua hatua kupunguza athari za kufungwa kwa shule ambapo asilimia 40 zimeongeza muda wa muhula wa masomo na kiwango hicho hicho zimepatia kipaumbele baadhi ya mitaala. Hata hivyo zaidi ya nusu ya nchi 142 zilizoshiriki kwenye utafiti zimesema hakuna marekebisho yoyote yatakayofanywa au yameshafanywa.
Nchi nyingi pia zimeboresha huduma za afya na viwango vya usalama wa kiafya katika vituo vya mitihani. Hata hivyo asilimia 28 ya nchi hizo zimefuta mitihani katika shule za sekondari za chini na aslimia 18 katika shule za sekondari za juu.
Kuhakikisha watoto wanaendelea kusoma hata katikati ya COVID-19, ripoti inasema nchi nyingie zilichukua hatua ya kuwezesha watoto kusoma wakiwa nyumbani kupitia redio, televiseni hasa katika nchi za kipato cha chini. Hata hivyo zaidi ya theluthi moja ya nchi za kipato cha chini na kati zimeripoti kuwa ni nusu ya wanafunzi wa shule za msingi ndio walifikiwa na huduma hiyo.
Andreas Schleicher ambaye ni Mkurugenzi wa masuala ya elimu na stadi OECD anasema “kuna umuhimu wa kuw ana ushahidi bora zaidi kuhusu ufanisi wa wanafunzi kufundishwa wakiwa majumbani, hasa katika mazingira magumu zaidi na kusaidia kuendeleza na kutunga sera za kujifunza kidijitali.”