Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni wakati wa nchi kutoa tathmini zao kuhusu wanavyoendelea na utekelezaji wa SDGs

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akihutubia Baraza Kuu la UN
UN Video
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akihutubia Baraza Kuu la UN

Ni wakati wa nchi kutoa tathmini zao kuhusu wanavyoendelea na utekelezaji wa SDGs

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkutano wa ngazi ya juu wa Siasa kuhusu Maendeleo Endelevu kwa kifupi HLPF ulioanza tarehe 6 mwezi huu wa Julai unaendelea hadi tarehe 15 ya mwezi huu katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani na pia kwa nijia ya Mtandao. 

Mwaka huu 2021 mkutano huu umejikita katika baadhi ya malengo kati ya yale 17 yaliyokusudiwa kuwa yametimizwa ifikapo mwaka 2030. Na miongoni mwa yanayojadiliwa ni lengo namba 3 linaloangazia afya njema na ustawi. 

Kuanzia hii leo tarehe 12, kupitia Mkutano huo ulioandaliwa na Idara ya Umoja wa Mataifa ya uchumi na maendeleo, DESA, nchi 44 zimepanga kuwasilisha tathmini zao za hiari za kitaifa au mipango yao ya kufanikisha Malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. 

Ingawa katika nchi hizo, si nyingi kutoka Barani Afrika zitakazowasilisha hatua zilizopigwa, lakini Rais wa Tanzania tayari ameeleza kwa wananchi wake hatua zilizopigwa katika lengo namba 3 hususani katika suala la afya ya mama na mtoto. Rais Samia Suluhu Hassan anaanza kwa kutambua uwepo bado wa udumavu wa watoto katika nchi yake ingawa idadi inaendelea kupungua, “tatizo hili Tanzania lipo. Udumavu wa watoto, watoto wenye uzito mwepesi, utapiamlo, matatizo haya tunayo lakini yanapungua jinsi tunavyokwenda. Na kwa nini yanapungua. Yanapungua kwa sababu nilipokuwa Makamu wa rais, nilijipa kazi ya kushughulika na sekta ya afya na nikashughulika na afya ya mama na mtoto. Kwenye afya ya mama na mtoto tulijielekeza sana kwenye ujengaji wa vitu vya afya na zahanati ili kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi na kwa kiasi fulani tumeweza lakini pia nikajiingiza kwenye suala hili la lishe nikaingia mikataba na wakuu wa mikoa na kila mkuu wa mkoa nilimtaka asimamie lishe kwenye mkoa wake. Mbaya zaidi kwenye ile mikoa ambayo tunaita ni mkoa ya vyakula ndio mikoa yenye kiasi kikubwa cha utapiamlo na udumavu. Kwa hiyo kwa kuingia mikataba na wakuu wa mikoa, nilikuwa nawabana na wameweza kupunguza hali hii kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo sasa nitaifanya hiyo kazi nikiwa katika kiti hiki cha Urais ambapo najua wakuu wa mikoa sasa wataenda kujituma zaidi ili kuondosha tatizo hili.” 

Na tatizo ni nini hasa linalofanya kuendelea kuwepo kwa udumavu wa watoto katika nchi ambayo inasifika kwa kutokuwa na tatizo la ukosefu wa chakula? 

“Suala kubwa ni elimu ndio tumegundua kwamba wakina mama wengi na familia nyingi zinakosa elimu za kulisha vizuri. Lakini pia kujipangia muda wa kulisha mtoto. Kwa hiyo ni suala la elimu ni suala la kuwaelewesha wakina mama na familia za upande ule na hiyo inafanyika vizuri sasa mategemeo yetu kwamba tutakwenda kupunguza kwa kiasi kikubwa suala hili la udumavu kwa sababu chakula kipo hakuna shida ya chakula kule.” Anasema Rais Samia. 

Na je, ni hatua gani imepigwa katika kupunguza vifo vya mama na mtoto? Rais Samia Suluhu Hassan anaeleza zaidi akisema, “katika kila sekta tunafanya kazi kuendana na Malengo ya SDGs. Katika kila sekta. Kwenye upande wa watoto kazi nzuri sana imefanyika. Tumepunguza utapiamlo lakini pia kutokana na huduma za afya zilizopo, tumepunguza sana vifo vya watoto. Miaka miwili mitatu nyuma tulikuwa na vifo 57 katika vizazi 1000, sasa hivi tuna vifo 7 katika vizazi 1000 kwa upande wa watoto. Lakini kwa upande wa akiana mama tulikuwa na vifo 500 na katika vizazi 100, 0000, sasa hivi tumeshuka tuko kwenye 320 hivi katika vizazi hai laki moja. Kwa hiyo tunakwenda vizuri.”