Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njaa ilikithiri mwaka 2020, COVID-19 moja ya kichocheo- Ripoti 

Wakulima nchini Madagascar na mbegu mpya kwa ajili ya kuongeza mazao.
UNEP/Lisa Murray
Wakulima nchini Madagascar na mbegu mpya kwa ajili ya kuongeza mazao.

Njaa ilikithiri mwaka 2020, COVID-19 moja ya kichocheo- Ripoti 

Afya

Hali ya njaa duniani ilizidi kuwa mbaya mwaka jana wa 2020, imesema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa hii leo ikisema kuwa hali hiyo inaweza kuwa ilisababishwa pia na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa kwa pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa ikiwemo lile la chakula na kilimo, FAO, mpango wa chakula duniani WFP, linalohudumia watoto, UNICEF, mfuko wa maendeleo ya kilimo, IFAD na lile la afya WHO inasema takribani watu milioni 811 duniani walikuwa hawana lishe bora mwaka jana, idadi ambayo iwapo itaendelea hivyo itakwamisha kufikia lengo la kutokomeza njaa duniani ifikapo mwaka 2030. 

Ikipatiwa jina Hali ya upatikanaji wa chakula na lishe duniani, ya kwanza kabisa tangu kuibuka kwa janga la COVID-19, utangulizi wake unaweka bayana kuwa matoleo yaliyotangulia tayari yalishaonya juu ya hatma ya mamilioni ya watu wengi wao watoto kupata chakula cha uhakika. 

“Bahati mbaya, janga la Corona linafanya hali iwe mbaya zaidi na kuonesha udhaifu wa mifumo ya chakula duniani ambayo inatishia maisha na mbinu za watu kujipatia kipato,” wamesema wakuu wa mashirika hayo matano katika utangulizi wa ripoti hiyo. 

Wakuu hao wanaonya kuwepo kwa hali ya mbaya zaidi huku wakionesha matumiani ya ongezeko la hatua za kidiplomasia kwa kuwa “mwaka huu kuna fursa ya kipekee ya kusongesha upatikanaji wa chakula na lishe bora kupitia mikutano ya ngazi ya juu ya mifumo ya chakula, ukuaji wa lishe na mkutano wa 26 wa mabadiliko ya tabianchi, COP26 ambapo matokeo ya vikao hivi yataumba nusu ya pili ya muongo wa Umoja wa Mataifa wa hatua dhidi ya lishe.” 

Takwimu zinasemaje? Bara la Asia lina watu wengi zaidi wenye njaa 

Tayari katikati ya miaka ya 2000, njaa ilianza kuongezeka na kutowesha matumaini ya kuondoa tatizo hlio. Cha kusikitisha zaidi miaka ya 2020 ilipoanza, njaa ikaongezeka kuzidi hata kiwango cha ukuaji wa idadi ya watu. Mwaka jana asilimia 9.9 ya wakazi wa dunia hawakupata lishe ya kutosha, kiwango ambacho ni cha juu ikilinganishwa na asilimia 8.4 mwaka uliotangulia wa 2019. 

Zaidi ya nusu ya watu wasio na lishe bora, sawa na watu milioni 415 wanaishi barani Asia. Zaidi ya theluthi moja wako Afrika ikiwa ni watu miioni 282. Nchi za Amerika kusini na Karibea kiwango ni kidogo milioni 60. 

Ingawa hivyo ongezeko zaidi la njaa lilikuwa barani Afrika ambako uwepo wa watu wenye lishe duni ni asilimia 21 ya wananchi wake, ikiwa ni maradufu kuliko eneo lolote lile. 

Utapiamlo umekithiri katika aina mbalimbali: Watoto ndio wanagharimika zaidi ambako mwaka 2020, zaidi ya watoto milioni 149 wenye umri wa chini ya miaka 5, huku milioni 45 ni wadumavu na milioni 39 wana unene kupindukia au matipatipwa. 

Wanawake nao wenye umri wa kubeba ujauzito wana ukosefu wa damu. Duniani kote, ingawa kuna maendeleo kwenye unyonyeshaji watoto, dunia bado haiku kwenye mwelekeo wa kufikia malengo ya lishe ifikapo mwaka 2030. 

Mkulima akivuna tufaha nchini Afghanistan.
World Bank/Rumi Consultancy
Mkulima akivuna tufaha nchini Afghanistan.

Vichocheo vya njaa 

Katika maeneo mengi duniani, janga la Corona limechochea mdororo wa uchumi na kuharibu uwezo wa watu kupata chakula. Hata kabla ya Corona, njaa ilikuwa imesambaa na hatua dhidi ya utapiamlo zilikuwa zinadorora. 

“Hali ilikuwa mbaya kwa mataifa ambayo yamekumbwa na mizozo na vita, hali mbaya ya tabianchi na hali nguvu ya uchumi pamoja na ukosefu wa usawa, vitu ambavyo kwa pamoja ripoti imevitaja kuwa vichocheo vya ukosefu wa uhakika wa chakula.” 

Kuna hatua za kuchukua 

Kama ilivyotajwa katika ripoti ya mwaka jana, kufanyia marekebisho mifumo ya chakula ni muhimu ili kuhakikisha kila mtu ana uhakika wa kupata chakula, kuboresha lishe na kuhakikisha kila mtu anapata mlo wa uhakika wenye lishe. 

Watunga sera wanatakiwa kujumuisha kwa pamoja sera za kibinadamu, maendeleo, ujenzi wa amani kule kwenye mizozo. Mathalani kuweka mikakati ya hifadhi ya jamii ili kuzuia familia kuuza rasilimali kidogo iliyo nayo ili kununua chakula. 

Halikadhalika kuimarisha mifumo ya chakula yenye mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, mathalani kupatia wakulima wadogo bima ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye mazao yao.