Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hata wakati wa COVID-19 huduma za afya ya uzazi ni muhimu si mbadala- UNFPA

Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dkt.Natalia Kanem akiwa amembeba mtoto mchanga katika wodi ya wazazi kwenye hospitali moja jimboni Blue Nile nchini Sudan. UNFPA inatoa huduma za afya ya uzazi za kukoa maisha katikati ya janga la COVID-19.
UNFPA Sudan/Sufian Abdul-Mouty
Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dkt.Natalia Kanem akiwa amembeba mtoto mchanga katika wodi ya wazazi kwenye hospitali moja jimboni Blue Nile nchini Sudan. UNFPA inatoa huduma za afya ya uzazi za kukoa maisha katikati ya janga la COVID-19.

Hata wakati wa COVID-19 huduma za afya ya uzazi ni muhimu si mbadala- UNFPA

Afya

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya idadi ya watu duniani, shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu, UNFPA limeangazia jinsi ambavyo janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 limeingilia na kutishia fursa ya watu kuchagua kuwa na watoto au la.

Katika ujumbe wake kwa njia ya video siku ya leo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dkt. Natalia Kanem amesema, “janga la COVID-19 limechochea baadhi ya watu kuahirisha suala la kuwa na mtoto. Kwa wengine, kuvurugika kwa huduma za afya ya uzazi kumesababisha wengine kubeba ujauzito ambao hawakupanga.”

Dkt. Kanem amesema mazingira hayo mawili yameibua wasiwasi mkubwa juu ya uwezekano wa ongezeko la watoto au kupungua kwa idadi ya watoto.

“Hata hivyo hofu kubwa inakuja pale ambapo watu hawawezi kuamua wao wenyewe kuhusu uchaguzi kuhusu miili yao na kile ambacho wanataka kufanya kuhusu masuala ya ngono na uzazi kutokana na kuvurugwa kwa huduma za afya ya uzazi,” amesema Dkt. Kanem.

Beatrice Sebastiao mwenye umri wa miaka 28, manusura wa fistula ya uzazi huko Mocuba, jimbo la Zambezia, Msumbiji
UNFPA Mozambique
Beatrice Sebastiao mwenye umri wa miaka 28, manusura wa fistula ya uzazi huko Mocuba, jimbo la Zambezia, Msumbiji

UNFPA inasema wakati wa janga la Corona, huduma za afya ya uzazi zinapuuzwa katika baadhi ya maeneo ambako zinaonekana kuwa siyo za muhimu. “Kuna hofu kuwa janga hili linaweza kutumiwa kama sababu ya kudhibiti au kuacha kusaidia wanawake na wasichana katika uamuzi wao wa kufikia huduma hizo kupitia vikwazo vya kutotembea.”

Utafiti wa UNFPA uliotolewa mwezi Machi mwaka huu ulionesha kuwa takribani wanawake milioni 12 walikumbwa na adha baada ya huduma za uzazi wa mpango kuvurugika kutokana na janga la COVID-19.

Ni kwa mantiki hiyo Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNFPA anatoa wito kwa siku hii kwa kila mtu kuchukua hatua kuziba pengo popote pale alipo la huduma za afya ya uzazi kwa kuwa ni muhimu na si suala la uchaguzi au mbadala.

“Janga la Corona linaweza kuchochea mtu kuchagua, lakini haki ya kuchagua iwapo kuwa na familia au la hiyo haibadiliki. Halikadhalika wajibu wa mfumo wa afya wa kulinda haki hiyo," ametamatisha Dkt. Kanem.