Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yataka dozi za chanjo ya Corona zizalishwe mara mbili zaidi ya sasa

Mhudumu wa afya nchini Ethiopia akijiandaa kumpatia mtu chanjo dhidi ya COVID-19.
© UNICEF/NahomTesfaye
Mhudumu wa afya nchini Ethiopia akijiandaa kumpatia mtu chanjo dhidi ya COVID-19.

UN yataka dozi za chanjo ya Corona zizalishwe mara mbili zaidi ya sasa

Afya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema dunia inahitaji angalau dozi bilioni 11 za chanjo ya ugonjwa wa Corona au COVID-19, ili kuweza kupatia asilimia 70 ya watu duniani na kuondokana na janga la Corona ambalo linaisumbua dunia kwa miaka miwili sasa. 

Akizungumza katika mkutano wa tatu wa mawaziri wa fedha na magavana wa Benki Kuu wa kundi la nchi 20 au G20, Guterres amerejelea tena wito wake wa kuanzishwa kwa mpango maalum wa chanjo duniani ili kuongeza uzalishaji angalau mara mbili ya sasa.  

“Pengo la chanjo ulimwenguni linatutishia sisi sote kwa sababu virusi vinavyobadilika, vinaweza kuwa vinaleta maambukizi zaidi na kufanya hali kuwa mbaya zaidi. Tunashukuru na kukaribisha ahadi za chanjo na fedha lakini hazitoshi. Tunahitaji angalau dozi bilioni kumi na moja kuchanja asilimia 70 ya ulimwengu na kumaliza janga hili.”

Halikadhalika amehimiza uwepo wa usawa katika usambazaji wa chanjo kwa nchi zote tajiri na masikini kupitia jukwaa la COVAX ili kupunguza utofauti mkubwa uliopo sasa wa nchi zilizochanja wananchi wake kwa idadi kubwa huku nchi nyingine idadi ikiwa ndogo au haijachanja kabisa. 

Katibu Mkuu Antonio Guterres akishiriki kwa njia ya video mkutano wa G-20 (Maktaba)
UN Photo/Evan Schneider
Katibu Mkuu Antonio Guterres akishiriki kwa njia ya video mkutano wa G-20 (Maktaba)


“Ulimwengu unahitaji Mpango wa Chanjo ya pamoja, angalau uzalishaji wa chanjo mara mbili na kuhakikisha usambazaji sawa, kwakutumia jukwaa la COVAX. Natoa wito kuwepo na kikosi cha dharura kitakacho jumuisha nchi zinazozalisha chanjo na zinazoweza kuzalisha, Shirika la Afya ulimwenguni -WHO, GAVI, pamoja na taasisi za kifedha za kimataifa ambazo zinaweza kushughulika na makampuni yanayotengeneza chanjo . naamini G20 inaweza kuandaa na kutekeleza mpango huu”

Katika hatua nyingine Guterres amezisihi nchi hizo za G20 kusaidia nchi zinazoendelea kwakuwa sasa zinakabiliwa na mzigo wa madeni hali inayofanya uchumi wa nchi zao uzidi kudidimia. Ameshauri nchi hizo tajiri duniani kuweka mifumo mizuri itayo ziwezesha nchi zinazoendelea kukopa na kupata maendeleo.