Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa waahidi kushirikiana na uongozi mpya wa Haiti

Waziri Mkuu wa Haiti Claude Joseph akizungumzia hali ya nchi yake katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa
UN Photo/Evan Schneider
Waziri Mkuu wa Haiti Claude Joseph akizungumzia hali ya nchi yake katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa

Umoja wa Mataifa waahidi kushirikiana na uongozi mpya wa Haiti

Amani na Usalama

Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti, Helen La Lime amekiri uhalali wa Waziri Mkuu Claude Joseph kuliongoza taifa hilo ambalo katikati ya wiki hii lilimpoteza rais wake aliyeuwawa akiwa nyumbani kwake. 

Lime amesema, Umoja wa Mataifa upo tayari kushirikiana na kiongozi huyo ambaye amechukua nafasi ya uongozi kwa mujibu wa katiba ya nchi na kukaribisha dhamira ya serikali hiyo inayo ongozwa na Claude Joseph kufanya uchaguzi wa kitaifa baadae mwaka huu. 

“Kiongozi huyu ambaye anashika madaraka ya kuiongoza Haiti katika kipindi hiki kwa mujibu wa sheria baada ya kifo cha rais wao yupo tayari kufanya mazungumzo na kuendelea na mchakato wa kufanya uchaguzi kulingana na kalenda ya uchaguzi ambayo ilitolewa wiki iliyopita” amesema Lime

Ratiba iliyotolewa hivi karibuni inaonesha duru ya kwanza ya uchaguzi inatarajiwa kufanyika tarehe 26 Septemba, na duru ya pili ikitarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu 2021. 

Raid Jovenel Moise wa Haiti aliuwawa siku ya jumatano tarehe 06 Julai 2021 akiwa nyumbani kwake na kikundi cha watu ambao bado hawajafahamika. 

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres alituma salamu za rambirambi kwa taifa la Haiti na kulaani mauaji hayo na pia kuwahimiza wananchi wa Haiti wawe watulivu na wasikubali kuliingiza taifa hilo katika machafuko kufuatia kuuwawa kwa rais wao.