Idhini ya kuvusha misaada ikikoma Julai 10, Wasyria watakuwa hatarini zaidi - OCHA 

8 Julai 2021

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya kibinadamu, OCHA, imeonesha wasiwasi wake kuwa ifikapo tarehe 10 mwezi huu wa Julai,  kushindwa kuongeza idhini iliyowekwa na Baraza la Usalama la UN ya kuvusha misaada ya kibinadamu kutaongeza viwango vya mateso kwa raia ambavyo ambavyo havijaonekana katika kipindi cha miaka 10 ya mgogoro wa Syria.

Video iliyorekodiwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya kibinadamu OCHA, inaanza kwa kuonesha magari makubwa ya mizigo yakiwa yamesheheni mizigo katika Kituo cha usafirishaji cha Umoja wa Mataifa nchini Uturuki.  

Mamilioni ya Wasyria wanategemea misaada ya UN inayotolewa chini ya idhini kutoka kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la pande zote za mpaka kuruhusu misaada hiyo kuvushwa. 

Mark Cutts, Naibu Mratibu wa masuala ya  Kibinadamu wa Kikanda kwa upande wa Mgogoro wa Syria katika Umoja wa Mataifa anasema, "kuna watu milioni 3.4 upande wa pili wa mpaka hapa, ambao tunawapa chakula, dawa, mahema, blanketi, na vifaa vingine vya msaada vinavyohitajika haraka. Kushindwa kuendeleza azimio la Baraza la Usalama kwa shughuli hii ya kuvuka mpaka itawanyima mamilioni ya watu ambao wamenaswa katika eneo la vita msaada ambao wanauhitaji kwa maisha yao." 

Muongo mmoja wa vita na kuanguka kwa uchumi kumewaacha zaidi ya watu milioni 13 nchini Syria wakihitaji msaada wa kibinadamu. Baadhi ya mahitaji muhimu zaidi yako kaskazini magharibi mwa nchi ambapo watu milioni 4.2 hasa wanawake na watoto, wamenaswa katika eneo la vita karibu na mpaka wa Syria na Uturuki. 

Katika kambi ya Kansafra, Idlib nchini Syria, kuna kituo cha afya ambacho angalau kimesalia kikisaidia watu. Mustafa Rahhal, ni Daktari hapa anasema, "ikiwa mpaka utafungwa itamaanisha kuzuia baraka kubwa. Wakati tu utakapofungwa tutapoteza baraka ya huduma ya afya, dawa, vifaa ambavyo vinatufikia, na wafanyakazi wa matibabu. Hii inamaanisha kuwa tutakuwa katika uhakika wa kufa" 

Operesheni ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Syria hivi sasa ni kubwa zaidi kuliko sehemu nyingine yoyote ulimwenguni. Kwa upande wa kaskazini magharibi, eneo nje ya udhibiti wa serikali ya Syria, UN inapeleka mpakani kutoka Uturuki malori 1,000 kila mwezi yakiwa na chakula, vifaa muhimu vya matibabu, chanjo ya COVID-19, na msaada mwingine wa kuokoa maisha. 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter