Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jukwaa la Usawa wa Kijinsia la Paris limekidhi matarajio yetu vijana - Abel Koka

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres ( wa pili kulia) akizungumza katika jukwaa la usawa wa kijinsia , Paris Ufaransa
MEAE/Jonathan Sarago
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres ( wa pili kulia) akizungumza katika jukwaa la usawa wa kijinsia , Paris Ufaransa

Jukwaa la Usawa wa Kijinsia la Paris limekidhi matarajio yetu vijana - Abel Koka

Malengo ya Maendeleo Endelevu

"Jukwaa la Usawa wa Kijinsia lililokamilika mjini Paris likiwakutanisha vijana pamoja na viongozi watoa maamuzi kutoka mataifa mbalimbali limekidhi matarajio yetu sisi vijana," hayo ni maneno ya Abel Koka wa shirika la Restless Development la Tanzania ambaye ni mmoja wa Kikosi Kazi cha vijana 40 wa kusongesha kizazi cha usawa wa kijinsia, kilichoundwa na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusiana na wanawake. 

"Kama vijana tunafurahi sana matarajio yetu tumeyapata kwa sababu tulikuwa tunatamani kuona vijana nao wanashiriki kwenye ngazi za maamuzi lakini pia kuelezea hisia zao na matamanio yao ya nini kifanyike ili usawa wa kijinsia uweze kupatikana. Na tumeona vijana wameweza kushiriki iapasvyo kwanza kwenye ufunguzi wa kongamano lenyewe, lakini pia kwenye mijadala mbalimbali ambayo iliendelea baada ya hapo. Kwa hiyo sauti za vijana zimesikika na maoni yao yamesikilizwa kwa kiasi kikubwa katika kongamano hilo." 

Na kuhusu ni kipi kikubwa zaidi kutoka kwa viongozi ambacho ameona ni ahadi mahususi na si maneno tu, Abel Koka anasema, 

(Sauti ya Abel Koka)

"Ahadi zilizotoka kwa viongozi kwa sasa, ninaweza kusema zilikuwa ni ahadi mahususi kwa sababu kwa mujibu wa takwimu ambazo zimetolewa ni kiasi cha dola za kimarekani bilioni 40 kimeahidiwa kwenda kuleta usawa wa kijinsia kwenye jamii na bilioni 40 hiyo inatoka kwenye mashirika mbalimbali ya maendeleo, lakini pia kwenye serikali mbalimbali kote duniani. kwa hiyo kwa sisi tulikuwa tunalilia sana rasilimali fedha kwa ajili ya kwenda kusukuma gurudumu la usawa wa kijinsia na tumeweza kuona mataifa na asasai zisizo za kiserikali na wadau wa maendeleo wametamka fedha ambazo watatoa kwenda kusukuma gurudumu la maendeleo. Kwa hiyo kinachotakiwa kifanyike sasa hivi ni kungalia ni kwa namna gani fedha hizo zitaweza kutumika kuweza kusukuma gurudumu la usawa wa kijinsia."

UN Women inasema uwekezaji wa dola bilioni 40 za kimarekani zilizothibitishwa kwenye mkutano huo zinaonesha hatua kubwa katika utoaji wa haki za wanawake na wasichana kwa kuwa ukosefu wa fedha unaeleweka kuwa sababu kuu ya maendeleo ya taratibu mno katika kuendeleza usawa wa kijinsia.

TAGS: Generation Equality, Abel Koka, Restless Development, Usawa wa kijinsia.