Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yasikitishwa na mauaji ya Rais wa Haiti

Rais wa Haiti Jovenel Moïse alipokuwa akihutubia mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la UN mwaka 2018
UN/Cia Pak
Rais wa Haiti Jovenel Moïse alipokuwa akihutubia mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la UN mwaka 2018

UN yasikitishwa na mauaji ya Rais wa Haiti

Masuala ya UM

Kufuatia taarifa za kuuawa kwa kupigwa risasi Rais wa Haiti, Jovenel Moïse, Umoja wa Mataifa umelaani vikali kitendo hicho kilichotokea leo kwenye mji mkuu Port-au-Prince.

Tweet URL

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake jijini New York, Marekani hii leo amesema, "nalaani vikali mauaji ya Rais Jovenel Moïse. Watekelezaji wa tukio hili lazima wafikishwe mbele ya sheria."

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa watu wenye silaha wasiojulikana wali-vamia nyumba yake mjini Port-au-Prince majira ya saa saba za usiku wa kuamkia leo Jumatano kwa saa za Haiti na kumpiga risasi ambapo mke wake pia amejeruhiwa.

Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa wananchi na serikali ya Haiti pamoja na familia ya hayati Moïse.

Halikadhalika ametoa wito kwa wananchi wa Haiti kuwa watulivu na wazingatie katiba wakati wa tukio hili la kuchukiza na wasikubali ghasia.

Amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake utaendelea kushikamana na serikali na wananchi wa Haiti.

Rais Jovenel Moïse amekuwa madarakani tangu mwezi Februari mwaka 2017 na aliingia kufuatia uchaguzi uliotokana na mtangulizi wake Michel Martelly kujiuzulu.

Baraza la Usalama la UN nalo lapaza sauti

Wakati huo huo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nalo limetoa taarifa yake kulaani mauaji ya Rais huyo wa Haiti.

Rais wa Baraza hilo Nicolas De Riviere ametoa taarifa mbele ya wajumbe hii leo wakati wa kikao chao cha asubuhi akisema, "napenda, kwa niaba ya wajumbe wa Baraza la Usalama kuelezea masikitiko juu ya kifo cha Rais

Jovenal Moïse wa Haiti. Wajumbe wa Baraza wanaelezea mshtuko wao mkubwa kufuatia taarifa za mauaji ya Rais Moïse yaliyotokea mapema leo huko Port-au-Prince na hofu yao kubwa sasa ni mustakabali wa Mke wa Rais aitwaye Martine Moïse ambaye naye pia alipigwa risasi wakati wa shambulio."

Wajumbe wa Baraza wanatuma salamu za rambirambi kwa familia ya Rais na kwa serikali na wananchi wa Haiti.