Watu 4,000,000 wafa kwa COVID-19, ni historia ya machungu- Guterres 

8 Julai 2021

“Hii leo dunia inaandika historia nyingine ya machungu katika vita dhidi ya ugonjwa wa Corona au COVID-19 kwa kufikisha vifo milioni 4 tangu COVID-19 kutangazwa janga la dunia mwezi Machi mwaka 2020,” ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyotoa leo. 

Guterres anasema idadi hiyo ya watu waliokufa kati ya watu 183,934,913 waliougua ugonjwa huo ni sawa na idadi ya watu katika nchi 1 kati ya 3 duniani kote. 

Katibu Mkuu amesema “wengi wetu tunatambua moja kwa moja vifo hivi na tuna machungu. Tunaomboleza vifo vya akina mama na akina baba ambao wametupatia mwongozo, wavulana na mabinti ambao wametuhamasisha, bibi na babu ambao walitupatia busara zao, wafanyakazi wenzetu na marafiki ambao walitunyanyua katika maisha yetu.” 

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema kuna matumaini, “chanjo zinatupatia nuru ya matumaini, lakini bado kuna wingu zito. Kasi ya virusi inazidi kasi ya mgao na usambazaji wa chanjo. Janga hilo ni dhahiri bado kuna safari ndefu ya kulimaliza, zaidi nusu ya vifo vimetokea mwaka huu pekee.” 

Mamilioni ya watu wako hatarini iwapo virusi hivi vitaendelea kusambaa kama moto wa nyika. Kadri vinavyozidi kusambaa, “tunashuhudia mnyumbuliko wake zaidi na uwezo wake wa kusambaa kwa urahisi na kuwa hatari zaidi na hata kuwa na uwezo wa kuzuia uwezo wa chanjo ya sasa kuvikabili.” 

 

Tuondoe pengo la mgao wa chanjo 

Katibu Mkuu anataka kuondolewa kwa pengo la mgao wa chanjo kwa kuwa hadi hivi sasa, takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO zinaonesha kuwa ni chanjo 2,988,941,529 zilizokwishatolewa lakini kwa nchi maskini kama vile barani Afrika idadi ya waliopata chanjo ni chini ya asilimia 1. 

Guterres anasema ili kukidhi mahitaji na kushinda virusi, dunia inahitaji Mpango wa Chanjo wa dunia  ambao “utaongeza maradufu uzalishaji wa chanjo na kuhakikisha mgao sawa kupitia mfumo wa Umoja wa Mataifa wa mgao wa chanjo, COVAX.” 

 Amesema mpango huo pia utaratibu utekelezaji na ufadhili wa fedha, na pia utasaidia nchi maskini ili ziwe tayari na pia ziwe na uwezo wa kuandaa mipango ya utoaji chanjo huku zikishughulikia changamoto ya watu kuhofia kupatiwa chanjo. 

“Kufanikisha mpango huo, ninatoa wito kuwepo kwa Kikosi Kazi cha dharura kinacholeta pamoja nchi zote zenye uwezo wa kutengeneza chanjo, WHO, fuko la chanjo duniani, GAVI na taasisi za fedha za kimataifa zenye uwezo wa kuwasiliana na kampuni za kutengeneza dawa na wadau wengine muhimu,” amesema Katibu Mkuu. 

 Amesisitiza kuwa uwiano katika mgao wa chanjo ndio jaribio la kimaadili kwa zama za sasa na pia kila mtu ataendelea kuwa katika tishio la kupata COVID-19 hadi pale kila mtu atakapokuwa amepatiwa chanjo. 

Guterres amekumbusha kuwa suala la dunia kujikwamua kutoka katika janga la Corona linawezekana pale kila mtu akiwa amepatiwa chanjo. “Vifo vya watu milioni 4 kutokana na janga hili lazima liwe kichocheo cha hatua za dharura za kumaliza janga hili kwa kila mt una kila mahali.” 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter